Niliwavisha sketi na ushungi watoto wangu wa kiume ili wasichukuliwe na Boko Haram-Mwathirika wa ugaidi

Wala Matari mwenye umri wa miaka 29, aliyewahi kuwa mateka wa magaidi, akiwa kanisani na watoto wake katika kijiji cha Zamai kilichoko kaskazini mwa Cameroon
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wala Matari mwenye umri wa miaka 29, aliyewahi kuwa mateka wa magaidi, akiwa kanisani na watoto wake katika kijiji cha Zamai kilichoko kaskazini mwa Cameroon

Niliwavisha sketi na ushungi watoto wangu wa kiume ili wasichukuliwe na Boko Haram-Mwathirika wa ugaidi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuelekea siku ya kimataifa ya kumbukizi ya manusura wa ugaidi, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi UNOCT imechukua hatua ya kupaza sauti za manusura hao kutoka maeneo mbalimbali duniani akiwemo mwanamke mmoja raia wa Cameroon ambaye anasema alilazimika kuwavisha mavazi ya kike watoto wake wa kiume ili wasichukuliwe na magaidi wa Boko Haram.

Taarifa ya mama huyu mcameroon aliyejaribu kuwavalisha mavazi ya kike watoto wake wa kiume ili wasichukuliwe na Boko Haram, inasimuliwa na Arnold Kayanda.

“Walikuja katikati ya usiku nilikuwa nimelala na watoto wangu na mume wangu. Walikuwa wamefunika nyuso zao wakiwa wameacha tu matundu kwenye eneo la macho yao. Walikuwa wanawakwapua tu watu, wanawafunga, wanawavua nguo.”

Mama huyu Mcameroon aitwaye Wala Matari anaeleza namna familia yake ilivyojikuta katika vurugu hizi zenye madhara mabaya zaidi katika nchi nne barani Afrika yaani Niger, Chad, Nigeria na Cameroon.

Mgogoro wa Boko Haram umewalazimisha maelfu kuyahama makazi yao. Wengi wanaishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Sehemu ya I: "Walinichapa hadi mimba ikatoka na kisha wakawa wananibaka"

Wala Matari anaishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamai iliyoko kaskazini wa Cameroon. Anasema magaidi walipovamia nyumbani kwake alijaribu kuwabadilisha watoto wake watano wa kiume kwa kuwavisha mavazi ya kike ili wasionekane kuwa ni wavulana. Lakini magaidi wa Boko Haram waliigundua janja yake na hivyo wakamlazimisha yeye na familia yao kuambatana nao kutoka kaskazini mwa Cameroon hadi Nigeria ambako waliishi kwa miaka miwili ya mateso makali ikiwemo kunyanyaswa kingono.

Bi Matari anasema wengi waliojaribu kutoroka waliishia kukamatwa, kukatwa masikio, matiti au kukatwa miguu na kuachwa wafe vichakani. Siku moja wanajeshi walikuja kuwaokoa, yeye na familia yake wakatembea kwa takribani siku mbili, usiku wakitembea, mchana wakijificha na hivyo ndivyo walivyokiepuka kifo.