Makumi ya maelfu ya wakimbizi kutoka Nigeria wamiminika Cameroon-UNHCR
Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR nchini Cameroon, limesema linaendelea kupokea wakimbizi kutoka Nigeria ambao wanakimbilia Cameroon kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kundi la Boko Haram. UNHCR imesema baadhi yao ni wameshakimbia nchi yao zaidi ya mara tano hadi kumi kwa sababu hawana njia nyingine zaidi ya kujinusuru ili kusaka usalama
Ni sauti za purukushani za wakimbizi walioko safarini kuelekea Cameroon wakitokea Nigeria, wakimbizi hawa wanaonekana na virago vyao, iwe kwenye mkokoteni au kichwani. Watoto, wanawake kwa wanaume wote lengo ni kusaka maeneo salama.
Wanakimbia machafuko kutoka eneo la Rann ilililoko kilometa saba kutoka kituo cha mpakani cha Cameroon. Mmoja wa wakimbizi hao kutoka Nigeria ni Kellou Maloum Modu.
(Sauti ya Modu)
“Wakati wanajeshi waliondoka, hatukuwa na namna nyingine isipokuwa kuondoka. Hatukuwa na chochote cha kujikinga kwa hiyo ilikuwa bora kuondoka.”
Naye Hebibi Toudjum aliwasili kutoka Rann na hakukosa simulizi ya walichoshuhudia.
(Sauti ya Hebibi)
“Boko Haram waliwaua watu wengi, tulifika hapa siku sita zilizopita.”
Wakimbizi wanawasili na kupokelewa na UNHCR ambayo inawapatia makazi katika kambi ya muda. Geert Van de Casteele ni mwakilishi wa shirika hilo nchini Cameroon.
(Sauti ya Casteele)
“Licha ya kwamba tuna changamoto nyingi, lakini tunawaleta watu zaidi na kwa sasa, wafanyakazi wenzangu wameweza kufanya mahesabu kwa muda mfupi ambapo katika kipindi cha miezi mitatu ijayo UNHCR itahitaji takriban kati ya dola milioni kumi na moja”.
Mwezi Januari mwaka huu wa 2019 Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na serikali ya Cameroon na wadau walitoa tangazo la mahitaji ya kibinadamu ambayo yanalenga nchi nzima, ikiwemo maeneo ambayo yameathiriwa na Boko Haram. Takriban watu milioni 4.3 kutoka Cameroon, wengi wakiwa ni wanawake na Watoto, wana mahitaji ya dharura.