Wanigeria waendelea kufurushwa Cameroon

20 Aprili 2018

Nyumbani ni moto,  na ugenini nako moto.

Ingawa wanakotoka wanakabiliwa na mashambulizi ya Boko Haram, raia wa Nigeria waliosaka hifadhi kaskaizni mwa Cameroon sasa wanalazimishwa kufungasha virago.

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema kuna hata walioingia Cameroon kusaka usalama na baada ya siku mbili wakafuruswha warejee nyumbani hususan jimbo la Borno.

Kupitia taarifa yake, UNHCR imesema ina wasiwasi mkubwa kwa tangu mwaka huu uanze, wanigeria 385 wamelazimishwa kurejea nyumbani.

Hali imekuwa mbaya zaidi ikisema kuwa  “tarehe 10 mwezi huu wa Aprili, wakimbizi na wasaka hifadhi 160 kutoka Nigeria walilazimishwa kurejea jimbo la Borno, eneo ambalo bado linashambuliwa zaidi. Raia hao wamekuwa wamesaka hifadhi kwenye wilaya ya Waza nchini Cameroon tangu mwaka 2014,” imesema taarifa ya UNHCR.

UNHCR imesema kulazimisha wakimbizi kurejea nyumbani ni kinyume na misingi ya kutotakiwa kufanya hivyo. 

Halikadhalika hatua hiyo kwa mujbu wa UNHCR inakwamisha maendeleo yaliyokwishapatikana ya Cameroon kuwapatia hadhi wasaka hifadhi kutoka Nigeria ambao wanakimbia mashambulizi ya Boko Haram.

TAGS: Boko Haram, Cameroon, Nigeria, Borno, UNHCR

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter