Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio kwenye ukumbi wa harusi Kabul laua watu 63, UN yataka hatua zaidi za ulinzi

Taswira ya hali ilivyokuwa kwenye ukumbi wa harusi wa Shahr-e-Dubai baada ya shambulio la tarehe 17 Agosti 2019 mjini Kabul
UNAMA/Fardin Waezi
Taswira ya hali ilivyokuwa kwenye ukumbi wa harusi wa Shahr-e-Dubai baada ya shambulio la tarehe 17 Agosti 2019 mjini Kabul

Shambulio kwenye ukumbi wa harusi Kabul laua watu 63, UN yataka hatua zaidi za ulinzi

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la kigaidi lililofanywa jana wakati wa sherehe ya harusi katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul ambapo watu 63 wameuawa na wengine zaidi ya 180 wamejeruhiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wake, ameeleza masikitiko  yake huku akituma salamu za rambirambi kwa wafiwa, serikali ya Afghanistan na wananchi wake na akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Kilichotokea kinatisha

Kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA ambao pia umelaani tukio hilo, idadi kubwa ya waliouawa na kujeruhiwa ni wanawake na watoto.

“Usiku wa tarehe 17 Agosti, mshambuliaji wa kujilipua alilipua kilipuzi kwenye ukumbi wa harusi wa Shahr-e-Dubai ulioko magharibi mwa Kabul ambako takribani watu 1,000 walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya sherehe ya harusi ya waislamu wa dhehebu la Shia,” imesema taarifa ya UNAMA ikifafanua kuwa hivi sasa kikundi cha haki za binadamu cha ujumbe huo kinachunguza zaidi kupata taarifa kamili.

Akizungumzia tukio hilo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Tadamichi Yamamoto amesema, “shambulio ambalo kwa makusudi linalenga raia ni tukio la kukasirisha na linachukiza kwa kuwa linaweza kuelezewa kuwa ni kitendo cha uoga cha kigaidi.”

Kushambulia raia kwa makusudi ni kiashiria cha uoga-UNAMA

Bwana Yamamoto ambaye pia ni mkuu wa UNAMA amelaani vitendo hivyo vya kushambulia raia kwa makusudi na ambavyo amesema vinalenga kujenga hofu miongoni mwa jamii ambayo tayari imekumbwa na madhila mengi.

Taswira ya hali ilivyokuwa kwenye ukumbi wa harusi wa Shahr-e-Dubai baada ya shambulio la tarehe 17 Agosti 2019 mjini Kabul
UNAMA/Fardin Waezi
Taswira ya hali ilivyokuwa kwenye ukumbi wa harusi wa Shahr-e-Dubai baada ya shambulio la tarehe 17 Agosti 2019 mjini Kabul

Ukumbi wa harusi ambako sherehe hiyo ilikuwa inafanyika, upo kwenye eneo lenye idadi kubwa ya waislamu wa madhehebu ya Shia ambao idadi yao ni ndogo.

UNAMA inasema kuwa imeshasajili matukio kadhaa ya mashambulizi ya makusudi dhidi ya watu washia.

“Kasi ya mashambulizi ya aina hii inadokeza kuwa hatua za sasa zilizowekwa kwa ajili ya ulinzi ni lazima ziimarishwe na wale ambao wanapanga matukio kama haya ni lazima wafikishwe mbele ya sheria,” amesema mkuu huyo wa UNAMA.

 Halikadhalika Bwana Yamamoto amesema Umoja wa Mataifa uko bega kwa bega na wananchi wa Afghanistani katika kusongesha mchakato wao wa amani ambao utamaliza vita na hatimaye kuleta amani ya kudumu.