Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, raia waliendelea kulengwa na kushambuliwa Afghanistan- UNAMA

Taswira ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul
UNAMA/Fardin Waezi
Taswira ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul

Hata wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, raia waliendelea kulengwa na kushambuliwa Afghanistan- UNAMA

Amani na Usalama

Ghasia zikiendelea kukumba maeneo mbalimbali ya Afghanistan, Umoja wa Mataifa umeendelea kuwa na hofu kubwa kutokana na raia kuendelea kuuawa katika kasi ya kutisha.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili huko Kabul na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, imesema vikundi vinavyopinga serikali viliendelea kulenga raia kwa makusudi wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhani.

UNAMA imesema vikundi hivyo vinatumia vilipuzi vya kutengeneza na katika mji mkuu Kabul pekee mashambulizi yao yalisababisha vido vya raia 100.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Tadamichi Yamamoto, amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akitaka vikundi hivyo viache tabia hiyo kwa kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa za kibinadamu, na kwamba vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Bwana Yamamoto ambaye pia ni mkuu wa UNAMA amesihi pande zote kinzani ziheshimj sheria za kimataifa na zilinde raia.

Amesema hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha mashambulizi dhidi ya raia.

Kwa mujibu wa UNAMA wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani mashambulizi yalisababisha vifo ikiwemo mauaji ya mwanazuoni wa kidini tarehe 24 mwezi Mei wakati akiwa eneo la kuabudu mjini Kabul na pia tarehe 2 mwezi huu mashambulizi dhidi ya wanafunzi wa madhehebu ya Shia.

Bwana Yamamoto amelaani vitendo hivyo akisema vinachukiza na kueneza hofu.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa mamlaka kupitia maazimio ya Baraza la Usalama kuhakikisha wanalinda raia.