Raia waendelea kuwa chambo mzozoni Afghanistan- Ripoti

10 Oktoba 2018

Wananchi wa Afghanistan wameendelea kuwa waathirika wa mapigano yanayoendelea nchini mwao ambapo idadi kubwa wameendelea kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mashambulizi yanayofanywa hususan na wapinzani wa serikali.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya kuhusu ulinzi wa raia katikati ya mzozo iliyotolewa leo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Afghanistan, UNAMA.

Ripoti hiyo ya kuanzia Januari 01 mwaka huu hadi tarehe 30 mwezi uliopita wa Septemba inasema viwango vya vifo na majeruhi vimesalia juu sawa na kipindi kama hicho mwaka jana ikimaanisha kuwa raia wanaendelea kuwa chambo katika mzozo huo kati ya serikali na wapinzani.

“Kulikuwa na waathirika raia 8,050 ambapo kati yao 2,798 walifariki dunia na wengine 5,252 walijeruhiwa, idadi ambayo ni sawa na mwaka jana,” imesema ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi ya kujilipua na kujitoa mhanga pamoja na vilipuzi vya kutengenezwa, IEDs ndivyo vilivyosababisha idadi kubwa ya mauaji miongoni mwa raia pamoja na majeruhi, ambapo matukio hayo yaliyotekelezwa zaidi na vikundi vilivyojihami.

Sababu nyingine kwa mujibu wa  UNAMA ni mashambulizi ya ardhini na masalia ya vilipuzi ardhini ambapo raia wasio na hatia walijikuta wakiathirika zaidi.

Kwa upande wa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mzozo nchini Afghanistan, ripoti inatana majimb oya Nangarhar, Kabul, Helmand, Ghazni na Faryab ikisema kwa mara ya kwanza jimbo la Nangarhar lilipiku jimbo la Kabul na kuwa la kwanza kwa kuwa na idadia kubwa ya waathirika raia kwenye mzozo huo.

 “Kila kifo cha raia kinaacha familia iliyochanganyikiwa, ikiomboleza na kuhaha kukubali ukweli wa kupoteza mpendwa wao na kila raia anayeachwa na ulemavu au anayejeruhiwa anasalia na machungu ambayo hayasimuliki,” amesema Danielle Bell, mkuu wa haki za binadamu UNAMA.

Akizungumzia takwimu hizo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Tadamichi Yamamoto amesema kwa kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwenye mzozo nchini humo, Umoja wa Mataifa unatoa wito tena wa kumaliza mzozohuo  haraka na kwa njia ya amani.

Ametaka pande zote zichukue hatua zozote zinazowezekana il ikulinda raia dhidi ya vitendo hivyo katili ikiwemo kuweka hatua madhubuti kuelekea kwenye amani.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter