Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi yazindua kampeni ya chanjo ya Ebola kwa wahudumu wa afya-WHO

Chanjo dhidi ya Ebola  kwa wahudumu wa afya  Mashariki mwa DRC  jimboni Kivu Kaskazini.
WHO-Eugene Kabambi
Chanjo dhidi ya Ebola kwa wahudumu wa afya Mashariki mwa DRC jimboni Kivu Kaskazini.

Burundi yazindua kampeni ya chanjo ya Ebola kwa wahudumu wa afya-WHO

Afya

Wizara ya afya ya umma na kudhibiti ukimwi ya Burundi imezindua kampeni ya chanjo dhidi ya virusi vya Ebola kwa wahudumu wa afya na wasaidizi wengine wa karibu.

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni WHO njanyo hiyo ilianza rasmi Jumanne Agosti 13 kwenye eneo la Gatumba mpakani mwa Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC.

Kampeni hii ya chanjo ya Ebola ni sehemu ya maandalizi ya serikali ya Burundi kwa ajili ya uwezekano wa kuzuka kisa cha Ebola.

Kampeni hii inatekelezwa chini ya usimamizi wa wizara ya afya ya umma na kudhibiti Ebola, kwa msaada wa shirika la afya duniani WHO. Na msaada wa kifedha wa kuendesha kampeni hiyo umetolewa na muungano wa chanjo duniani GAVI.

Burundi imepokea dozi za chanjo ya Ebola aina ya rVSV-ZEBOV kuwalinda waauguzi hao dhidi ya virusi vya Ebola aina ya Zaire ambavyo imeiathiri DRc hivi sasa.

Kuhusu chanjo hiyo

Shirika la WHO linasema ingawa chanjo hiyo bado iko kwenye majaribio, haijaidhinishwa wala kuruhusiwa kuuzwa , imedhihirisha inafanya kazi na ni salama wakati wa mlipuko wa Ebola uliozuka Afrika Magharibi na utafiti zaidi unahitajika kabla haijaidhinishwa na kupewa leseni.

WHO inasema chanjo hiyo inatolewa kwa sababu za kibinadamu , kuwalinda wahudumu wa afya na walio msitari wa mbele katika hatari zaidi ya kuambukizwa mlipuko ukizuka na kwenye maeneo yaliyo na hatari zaidi ya maambukizi.

Mfano wahudumu wa afya wanaofanya kazi mipakani , lakini pia watu ambao kazi zao zinawaweka hatarini wakiwemo wafanyakazi wa maabara, wachunguzi na wale wanaoendesha shughuli za mazishi.

Kuwachanja watu haw ani muhimu sana na ni hatua bora ya maandalizi dhidi ya ugonjwa huo amesema Dkt. Kazadi Mulombo, mwakilishi wa  WHO nchini Burundi na kuongeza kuwa  "Chanjo ililinda Maisha ya watu wengi dhidi ya Ebola ilipoendeshwa kwa majaribio nchini Guenea mwaka 2015 na Burundi tutaitumia chanjo hiyo kwa minajili ya kujikinga.”

Hakuna kisa chochote cha ebola kilichoripotiwa Burundi lakini maandalizi ni muhimu sana ameongeza Dkt. Mulombo.

WHO ambayo inaisaidia Burundi katika maandalizi imetoa msaada wa kiufundi na pia vifaa muhimu vinavyohitajika kuendesha kampeni hiyo ikiwemo kuboresha maabara.

Pia WHO inaisaidia serikali katika kuishirikisha jamii, kuzijengea uwezo  kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti  maambukizi na visa na pia kusambaza taarifa kuhusu Ebola kupitia vyombo vya Habari.