Ingawa hakujaripotiwa visa vipya, Ebola bado ni tishio DRC:WHO

22 Februari 2019

Katika wiki tatu zilizopita hakujaripotiwa visa vipya vya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo , DRC, ambayo ni habari Njema kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni WHO. Hata hivyo shirika hilo limeonya kwamba ugonjwa huo bado ni hatari na unaendelea kwa mwenendo wa wastani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo msemaji wa WHO Tarik Jašarević amesema hadi kufikia tarehe 20 ya mwezi huu jumla ya visa vya Ebola nchini DRC ni 853 kati ya hivyo 788 vimethibitishwa na 65 vinashukiwa.

Hali halisi ya Ebola

Jašarević ameongeza kuwa maeneo ya Katwa na Butembo yanasalia kuwa yakutia wasiwasi wa kiafya kutokana na ugonjwa huo, lakini amesema katika ,maeneo mengine hali ni ya kutia matumaini na haya ni mafanikio makubwa ukizingatia kiwango cha mlipuko hapo awali katika maeneo haya.

Amesisitisita kuwa hata hivyo viashiria vingine kama “kuendelea kuwepo kwa idadi kubwa ya vifo, kuchelewa kubaini visa na kuwepo kwa idadi ndogo ya visa miongoni mwa watu wanaochunguzwa ni ishara ya hatari kubwa ya mzunguko wa kutokea maambukizi katika jamii zilizoatthirika.”

Kwa mujibu wa WHO timu za kukabiliana na ebola ni lazima ziendelee kuchukua tahadhari ya hali ya juu katika maeneo yote ambako visa vinapungua na kufuatilia watu waliohusika kubaini maambukizi mapya, sawa kama ilivyo katika maeneo ambako Ebola bado inasambaa , kubaini haraka visa hivyo na kuzuia kuendelea kwa maambukizi.

Mipango ya kuzuia usambaaji wa Ebola

Shirika la WHO pia limesema kituo cha kuratibu mipango ya kupambana na Ebola sasa kimehamishiwa Goma kutoka mji mkuu Kinshasa ili kuwa karibu na maeneo yaliyoathirika na mlipuko wa ugonjwa huo na kwamba shughuli za kuukabili zinaendelea kwa nguvu zote kwenye eneo la Beni. Goma itakuwa pia kituo cha kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na hatimaye baadaye kuendelezwa na kuwa kitengo maalumu cha kukabiliana na ebola.

Mapendekezo ya kukabiliana na mlipuko

Mamlaka ya kitaifa ya udhibiti ya DRC na Kamati ya Maadili wameidhinisha matumizi ya chanjo ya Ebola ya majaribio kwa kina mama wenye ujauzito wa zaidi ya miezi mitatu ikimaanisha ni katika hatua ya pili au ya tatu ya ujauzo wao, pia kwa kina mama wanaonyonyesha na Watoto walio na umri wa chini yam waka mmoja.

WHO inasema mama mjamzito akipata Ebola inasababisha hatari kubwa ya kifo au kupoteza mtoto, hivyo mabadiliko haya yatasaidia kuwalinda kina mama wajawazito ambao hapo awali walilindwa tu endapo watu waliowazunguka katika jamii walipatiwa chanjo.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter