Rais wa Baraza Kuu akutana na wanawake, wasichana na Watoto kambini Zaatari

23 Julai 2019

Mapema leo Jumanne asubuhi Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa amezuru kambi ya wakimbizi ya Zaatari nchini  Jordan. Kambi hiyo iliyo karibu na mpaka baina ya Syria na Jordan katika upande wa Kaskazini, ni maskani ya wakimbizi takriban 80,000 na karibu asilimia 20 ya kaya zote kambini zinaendeshwa na wanawake.

Bi. Espinosa akiwa kambini hapo amekutana na wasichana wanaoshiriki kundi la kusoma na pia kutembelea kituo kilichopo kambini hapo ili kufahamu zaidi kuhusu mradi ya kujifunza kwa njia ya mtandao ambao unawasaidia wakimbizi hao kupata ujuzi na mafunzo ya kompyuta.

Rais huyo wa Baraza Kuu alilakiwa na ujumbe kutoka mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la mpango wa chakula WFP na la kuhudumia Watoto UNICEF ambayo yanafanyakazi ya kutoa misaada na huduma kambini hapo na kupata nao mlo wa mchana kambini kabla ya kutembelea mtambo wa nishati ya jua au sola na kukutana na muoka mikate na fundi cherahani kwenye soko kubwa la kambi hilo lijulikanalo kama  “Shams Elyses”.

Jana Jumatatu Bi. Espinosa alikutana na kina mama wa kundi la kazi za sanaa la Safi ambalo linasaidia jamii yao kwa kutengezena vitu mbalimbali ikiwemo kushona nguo na ili kuchagiza uwezeshaji wa wanawake na kupambana na umasikini.

Kabla ya kutoa mguu kambini Zaatari Rais huyo wa Baraza Kuu alitembelea mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women wa Oasis, ambao lengo lake ni kuwawezesha wanawake wakimbizi wa Syria kwa kuwapa fursa za kiuchumi na kuwajumuisha katika Maisha ya jamii.

Washiriki katika mradi huo wanapewa mafunzo ya lugha, taarifa mbalimbali ya masuala muhimu kama ya afya, ukatili wa kijinsia na kingono, huduma ya watoto wadogo na fursa ya kufanyakazi kwa malipo.

Bi. Espinosa alitembelea pia karakana ya ushonaji na shule ya chekechea ambako alipata fursa ya kuzungumza na Watoto na wazazi kuhusu Maisha ya kambini zaatari.

Kupitia ukurasa wake wa tiwtter Rais huyo wa Baaraza kuu amewashukuru wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao wanafanyakazi kwa ushirikiano na serikali ya Jordan kutoa msaada, ulinzi, elimu na fursa ya huduma kwa wakimbizi kambini Zaatari. Bi. Espinosa atahitimisha ziara yake nchini Jordan kesho Julai 24.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter