Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wakimbizi wenye ulemavu Za'atari kucheza na wenzao bila woga

kambi ya wakimbizi ya Za'atarinchini Jordan inayoonekana kutoka juu.Ina wakimbizi kutoka Syria.
UN Photo/Mark Garten)
kambi ya wakimbizi ya Za'atarinchini Jordan inayoonekana kutoka juu.Ina wakimbizi kutoka Syria.

Watoto wakimbizi wenye ulemavu Za'atari kucheza na wenzao bila woga

Utamaduni na Elimu

Watoto wakicheza na kuimba katika uwanja huo jumuishi wa michezo unaotumiwa na watoto wakimbizi wenye ulemavu na wasio na ulemavu kama sehemu ya juhudi za kitaifa nchini Jordan za kufanya elimu inakuwa jumuishi kwa kila mtu.

Uwanja huu umewekewa vifaa maalum vya michezo vya  kuimarisha ubunifu kwa mtoto ikiwemo spika na marimba kwa watoto wenye tatizo la mishipa ya fahamu na shimo la mchanga na turubali la sarakasi kwa ajili ya watoto wenye usonji. Wengine wakicheza kwenye turubali la sarakati wengine wanacheza ngoma.

Miongoni mwao ni Asma mwenye umri wa miaka 8. 

 “ Tulipowasili hapa tulianza kucheza. Tulicheza na kuruka na tukafurahi. Tofauti ni turubali. Viwanja vingine havina turubali isipokuwa uwanja huu.”

Mwakilishi wa UNICEF nchini Jordan, Robert Jenkins, amesema kuwa katika jamii ambazo zimeathirika na migogoro, watoto wenye ulemavu ni miongoni mwa wale wanaosahauliwa sana, na bado wako hatarini kuweza kupuuzwa katika msaada wa kibinadamu.

Ameendelea kuwa kazi yao na serikali ya Jordan ya kujenga mifumo ya elimu jumuishi imewezesha watoto zaidi ya 4,000 kuanza masomo katika shule za umma katika jamii waliko na pia katika kambi za wakimbizi tangu mwaka wa 2012.

UNICEF inasema ufunguzi wa uwanja huo unatoa nafasi bora hapo baadaye ambapo watoto wote wanaweza kushiriki huku wakipata elimu na pia kucheza.

Takriban asilimia 30 ya wakimbizi wa Syria walioko nchini Jordan, wanamahitaji maalum ya kimwili au kiakili.

Mradi huu ulibuniwa na kutekelezwa na mshirika wa UNICEF nchini Jordan, Mercy Corps na umezingatia viwango vya kimataifa.

UNICEF inasema ni matarajio yake kuwa uwanja huo utakuwa kama kielelezo kwa viwanja vingine katika shule nyingi nchini Jordan.

UNICEF Jordan inasaidiwa na mashirika ya misaada ya Uingereza, Korea Kusini na Ausralia ili kuhakikisha maeneo katika kambi za wakimbizi nchini humo ikiwemo shule, vyoo pamoja na viwanja vya michezo vinafaa kutumiwa na watoto wenye ulemavu.