Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa amani unaojumuisha wanawake ni kitovu cha amani endelevu Afghanistan- Bi. Mohammed

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed, (kushoto) akizungumza na Rula Ghani ambaye ni mke wa rais wa Afghanistan mjini Kabul. (20 Julai 2019)
Fardin Waezi/UNAMA
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed, (kushoto) akizungumza na Rula Ghani ambaye ni mke wa rais wa Afghanistan mjini Kabul. (20 Julai 2019)

Mchakato wa amani unaojumuisha wanawake ni kitovu cha amani endelevu Afghanistan- Bi. Mohammed

Amani na Usalama

Chonde chonde wananchi wa Afghanistan fikieni maridhiano ya yaliyopita na muwajumuishe wanawake kwenye harakati zote za mchakato wa amani ya kudumu na sauti zao kwenye mchakato wa kisiasa zisikike, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed.

Bi. Mohammed amesema hayo leo kwenye mji mkuu wa Afghastan, Kabul wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara yake ya siku mbili nchini humo akiwa ameambatana na viongozi wengine wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akitembelea maonyesho kwenye kituo cha kumbukizi na mashauriano cha Afghanistan kilichopo kwenye mji mkuu Kabul. (20 Julai 2019)
Fardin Waezi/UNAMA
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akitembelea maonyesho kwenye kituo cha kumbukizi na mashauriano cha Afghanistan kilichopo kwenye mji mkuu Kabul. (20 Julai 2019)

Ziara yao ya siku mbili ilianza jana huko Kabul na kisha mjini Barmyan ambapo Bi. Mohammed alikuwa ameambatana na Mkuu wa Idara ya Siasa na Ujenzi wa amani ya Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA Natalie Kanem na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women Phumzile Mlambo-Ngcuka.

Lengo ya ziara hiyo iliyokuwa na viongozi wakuu wanawake pekee, lilikuwa ni kuonyesha mshikamano na wanawake wa Afghanistan katika masuala ya amani na usalama.

“Tumefika hapa kabla ya uchaguzi wa rais ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, lakini pia kuonesha mshikamano wetu kwenye mchakato wa amani ambao ni muhimu sana kwa mustakabali na uendelevu wa juhudi zote na matarajio ya serikali na wananchi wa Afghanistan,” amesema Naibu Katibu Mkuu.

Licha ya ghasia nchini Afghanistan, mchakato wa amani ya Afghanistan unaendelea ambapo hivi karibuni mazungumzo yamefanyika huko Qatar kwa pande mbili hasimu ambazo ni serikali na wataliban wakitoa wito wa ghasia zikome hususan zile zinazohusisha raia.

Ghasia za karibuni ni pamoja na shambulio la bommu nje ya Chuo Kikuu cha Kabul ambapo watu 10 waliuawa na wengine 33 walijeruhiwa.

Bi. Mohammed akazungumzia pia uwezeshaji wanawake akisema kuwa, “mwishoni mwa ziara hii ya siku mbili nimevutiwa sana na uongozi katika ngazi zote kuanzia Kabul hadi mashinani ambapo nimeshuhudia uwekezaji kwa rasilimali watu hususan wanawake.”

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed, (kati-kushoto) wakati wa mkutano na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani, (kati-kulia) mjini Kabul. (20 Julai 2019)
Fardin Waezi/UNAMA
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed, (kati-kushoto) wakati wa mkutano na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani, (kati-kulia) mjini Kabul. (20 Julai 2019)

Wakati wa ziara hiyo siku ya Jumamosi, ujumbe huo wa ngazi ya juu ulikuwa na mazungumzo na Rais Ashraf Ghani na mtendaji mkuu wa serikali Abdullah Abdullah na pia walikutana na vikundi mbalimbali vya wanawake, mkutano ambao uliandaliwa na Rula Ghani ambaye ni mke wa Rais wa Afghanistan.

 “Mazungumzo yangu ya uso kwa uso na wanawake wakati wa ziara  yangu yamenidhihirishia kuwa wanawake wako katika dhimay a uongozi, utoaji maamuzi na wanafahamu kabisa pale wanataka kwenda na kile wanahitaji kama msaada kutoka kwetu,” amesema Bi. Mohammed.

Ameongeza kuwa wamesikia kutoka kwao kuhusu masuala ya uchaguzi, kuwa ni lazima uwe halali, ufanyike kwa wakati, uwe jumuishi na sauti za wanawake lazima zisikike.

Tweet URL

Naibu Katibu Mkuu amesema kuhusu mchakato wa amani, “lazima uwe jumuishi na jumuishi ina maana kuwa wanawake lazima wawe kitovu pale ambapo inatakiwa kushughulikia mahitaji ya manusura wa ukatili.”

Amesisitiza kuwa huwezi kushughulikia amani na uendelevu, iwapo hautakubali kufikia maridhiano na masuala yaliyopita.  “Kwa hiyo hii imekuwa fursa nzuri sana kwetu na wakati wa ziara  yetu tumeshuhudia na kuridhika na manufaa ya uwekezaji uliofanywa na Umoja wa Mataifa na wadau wake kwa miaka kadhaa.”

Mapema aleo walisafiri hadi jimbo la Bamyan, ambako UNFPA inasaidia miradi kadhaa kwa ajili ya afya ya uzazi kwa wanawake na familia zao pamoja na kukabili ukatili wa kijinsia.

Walitembelea pia eneo ambako Umoja wa mataifa inategua mabomu, eneo ambalo linatambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO kama eneo la urithi wa dunia.

Eneo hilo la mabuda wa Barmyan lilishambuliwa kwa baruti na kuharibiwa na watalibani mwezi Machi mwaka 2001.

 

Nabu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kulia) akizungumza na mmoja wa wategua mabomu huko Barmyan nchini Afghanistan. (21 July 2019)
Fardin Waezi/UNAMA
Nabu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kulia) akizungumza na mmoja wa wategua mabomu huko Barmyan nchini Afghanistan. (21 July 2019)

Ainisho la wanawake kuhusu amani ni muhimu- Bi. Mlambo-Ngcuka

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amezungumzia kile ambacho amesikia kutoka kwa wanawake wa Afghanistan hususan uongozi kandamizi wakati wa utawala wa watalibani, utawala ambao ulizuia wanawake wasiende shule, wasifanye kazi wala wasizungumze hadharani au wasitoke nyumbani bila ya mwanaume.

"Lakini wanawake hawa hawa hivi sasa chini ya miradi inayoendeshwa na Umoja wa Mataifa wameweza kwa ujasiri sasa kupaza sauti zao wakielezea vipaumbele ." amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Women.

Hata hivyo amesema "wakati mazingira ya sasa yanazidi kushamiri kwa ajili ya mazungumzo ya amani na watalibani, suala la kuhakikisha kuwa wanawake wana ushiriki kamilifu kwenye mchakato huo pamoja na ule wa maridhiano na hatimaye uchaguzi ni muhimu sana kuliko wakati wowote ule."

Amesema wanawake lazima waweze kutekeleza haki yao ya kuainisha neno amani kwa maisha yao na wawe na kiti kwenye meza ya mazungumzo kuhusu mustakabali wa taifa lao akisema kuwa, "ni kwa kufanya hivyo tu ndio tutaweza kushuhudia kushamiri kwa amani na demokrasia nchini Afghanistan."

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akitembelea maonyesho kwenye kituo cha kumbukizi na mashauriano cha Afghanistan kilichopo kwenye mji mkuu Kabul. (20 Julai 2019)
Fardin Waezi/UNAMA
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akitembelea maonyesho kwenye kituo cha kumbukizi na mashauriano cha Afghanistan kilichopo kwenye mji mkuu Kabul. (20 Julai 2019)

Kutokomeza ukatili wa kingono na kijinsia Afghanistan ni wajibu wetu sote- Bi. Kanem

Miongoni mwa miradi ambayo Umoja wa Mataifa inasaidia nchini Afghanistan ni ule wa kutokomeza ukatili wa kijinsia na kingono kwenye majimbo ya Barmyan, Nangarhar na Kabul unaotekelezwa kupitia mfumo wa vituo vya afya vya familia vilivyomo ndani ya hospitali.

Mradi huu ulianzishwa mwaka 2011 kwa ushirikiano kati ya Wizara ya afya ya umma ya Afghanistan na UNFPA kufuatia utafiti katika majimbo hayo ulioonesha kuwa idadi kubwa ya wanawake walikuwa wanafika vituoni kusaka usaidizi dhidi ya vitendo vya ukatili.

"Licha ya machungu makali, mnepo wa wanawake na wasichana niliokutana nao wakati wa ziara, vimenipatia matumaini kuhusu mustakabali wa Afghanistan," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Natalie Kanem.

Amesema UNFPA imejitolea kuboresha afya na ustawi wa wanawake wa Afghanistan kwa kuweka msingi wa maisha ya kuchagua na usawa.

"Tunasonga mbele lakini safari bado ni ndefu. Ni pale tu ambapo wanawake watakuwa salama na wamewezeshwa kufanya maamuzi yao kuhusu miili yao na maisha yao, ndipo nchi itaweza kufanikisha maendeleo na amani endelevu," amesema Bi. Kanem.