Licha ya machafuko UN yataka wapiga kura kuhakikishiwa haki yao Afghanistan

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA unasema licha ya uchaguzi wa bunge hii leo kughubikwa na ghasia umetiwa moyo na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kutekeleza haki yao ya msingi ya kupiga kura na kutaka hakikisho kwa wote kuweza kupiga kura.
Katika taarifa iliyotolewa na UNAMA mjini Kabul , ujumbe huo umesema k, kwa kuwa uchaguzi huu ndio wa kwanza tangu mwaka wa 2001 kusimamiwa na Wafghanistan wenyewe , ni uchaguzi muhimu sana katika mchakato wa nchi hiyo kuelekea kujitegemea.
Mpango huo umesema mamilioni ya wananchi walijitokeza kwa wingi leo na kusubiri kwa muda mrefu katika foleni ili kuweza kupiga kura licha ya machafuko kadhaa yaliyojitokeza na matatizo ya kiufundi, katika tumeya uchaguzi.
Taarifa ya UNAMA imewapongeza wananchi waliopiga kura kwa kutekeleza haki yao ya kiraia na kuwataka wale wote waliokosa fursa ya kupiga kura kutokana na matatizo ya kiufundi ya tume ya uchaguzi nao wapewe nafasi ya kutimiza haki yao ya msingi kuchagua wawakilishi wao.
Mpango huo pia umesema unatambua hatua za haraka zilizochukuliwa na tume ya uchaguzi ya Afghanistan kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kupiga kuraatakayekosa fursa hiyo kutokana na matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza, pia serikali imesema kwa vituo ambavyo havikuweza kufunguliwa hii leo basi vitafunguliwa kesho ili zoezi hilo liweze kukamilika.
Na kwa wapiga kura wa Kandahar ambako uchaguzi uliahirishwa kwa sababu za kiusalama, UNAMA imesema watawezeshwa kupiga kura siku ya jumamosi ijayo .
Hata hivyo duru za habari zinasema ghasia zilighubika baadhi ya maeneo ya kupigia kura na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 28 na wengine kujeruhiwa.
Uchaguzi huu ambao ni muhimu umeshuhudia hatua mbalimbali zikiwemo za kuzuia uibaji wa kura na kuhusisha wachunguzi na wawakili wa wagombea takriban 400,000 ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki.
Umoja wa Mataifa umewahimiza wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya kisiasa pamoja na wapiga kura kuchangia katika kulinda mchakato wa uchaguzi hususan wakati wa kukusanya na kuhesabu kura. Na kwa mtu yreyote atakayekuwa na walakini wa uchaguzi basi awasilishe malalamiko yake kwa tume ya uchaguzi na tume inayoshughulikia malalamiko ya uchaguzi.
Na endapo madai ni ya msingi basi sheria ishike mkondo wake kwa kufanyika kwa uchunguzi na inapohitajika wahusika wawajibishwe.