Mashirika ya UN yatoa wito wa kutokomeza utapiamlo kwa watoto

14 Julai 2019

Katika kuelekea siku ya kuzinduliwa kwa ripoti ya hali ya usalama wa chakula na lishe duniani, taarifa iliyochapishwa  jumapili ya leo katika ukurasa wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya dharura, OCHA, imeeleza kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, yametoa wito wa kutokomeza mateso kwa watoto yanayotokana na utapiamlo. 

Wakuu wa mashirika ya Umoja, lile la chakula na kilimo FAO, la afya duniani WHO, la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la kuhudumia watoto UNICEF, mpango wa chakula WFP na ofisi ya misaada ya dharura OCHA, kupitia azimio lao pamoja wamesema, “wote tumeona hali ya mtoto mwenye utapiamlo mkali ambaye kupumua tu ndiyo dalili pekee ya maisha kwake. Tuliguswa wote wakati ambapo mtoto hakuweza kuokolewa.”

Kila mwaka, Umoja wa Mataifa unawapatia watoto milioni kumi wenye utapiamlo mkali, huduma wanayohitaji ili kuweza kurejea katika hali yao. Huduma hizi ni pamoja na lishe, matibabu ya maambukizi, kama vile magonjwa ya kuhara, usafi na huduma za kujisafi na pia maji ya kunywa na chakula bora cha lishe kwa ajili ya kuboresha afya.

Wanawake milioni mbili wajawazito waliokuwa na utapiamlo na pia akina mama waliojifungua walipokea dawa za virutubisho lishe ili kuboresha lishe yao nay a watoto wao. Umoja wa Mataifa pia unawasaidia mamilioni ya watoto wengine kila mwaka ili wasipate utapiamlo.

Watoto milioni 50 chini ya umri wa miaka mitano wana utapiamlo mkali

“Pamoja na muongo mmoja wa kupungua kwa utapiamlo, idadi ya watu wanaotaabika na njaa duniani imeongezeka katika miaka ya hoivi karibuni,” wameeleza wakuu wa FAO, WHO, UNHCR, UNICEF, WFP na OCHA.

Taarifa hiyo ya OCHA imeendelea kueleza kuwa watu milioni 820 kote duniani wanaatabika na njaa na takribani watoto milioni 50 chini ya umri wa miaka mitano wanaati ika na utapiamlo mkali ambao unaendana na kuwa chini ya uzito unaostahili ikilinganishwa na urefu wao. Na watoto milioni 149 wamedumaa na hawakui kiakili kutokana na utapiamlo.

Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yamesema yanafanya kazi kuweka mazingira ya kuhakikisha kunakuwa na uapatikanaji wa huduma ya afya na lishe wakati wote na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa familia zenye watoto wenye utapiamlo mkali wanaweza kupata matibabu ya kuokoa maisha zikiwemo  huduma za kiafya zilizoko katika mazingira yao badala ya kulazimika kusafiri mamia ya kilomita kuwapeleka watoto hospitali.

Kutokana na kwamba migogoro imekuwa ikichangia kuongezeka kwa njaa na utapiamlo katika miaka ya hivi karibuni, Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakitoa huduma zake katika mazingira magumu.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa unasema unasimama imara kuzisaidia nchi wanachama katika kuendeleza na kurekeleza sera zao, programu na mikakati ya kutokomeza mzigo wa utapiamlo wa aina zote. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud