Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda imewekeza dola milioni 18 kujianda dhidi ya ebola

Chanjo dhidi ya Ebola  kwa wahudumu wa afya  Mashariki mwa DRC  jimboni Kivu Kaskazini.
WHO-Eugene Kabambi
Chanjo dhidi ya Ebola kwa wahudumu wa afya Mashariki mwa DRC jimboni Kivu Kaskazini.

Uganda imewekeza dola milioni 18 kujianda dhidi ya ebola

Afya

Serikali ya Uganda na wadau wengine wamewekeza dola milioni 18 kwa ajili ya kujiandaa kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Taarifa za shirika la afya ulimwenguni, WHO zinasema fedha hizo ni kwa ajili ya kuandaa mikakati mbali mbali ikiwemo kuwandaa watoa huduma wa afya 526 katika wilaya 14 waliopatiwa mafunzo kuhusu namna ya kuhudumia watu wanaoshukiwa kuwa na ebola huku wakijikinga.

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Uganda vituo vya kutibu wagonjwa wa Ebola vimekarabatiwa ambako watoa huduma wanapokea mafunzo ya kuhudumia wagonjwa katika wilaya za Kasese (Bwera), Bundibugyo, Wakiso (Entebbe), Kabarole, Kikuube and Ntoroko na vituo vingine viwili vinakarabatiwa katika wilaya ya Kanungu district na Naguru mjini Kampala. Pia kumekarabatiwa vituo vya kutengwa katika wilaya za Arua, Gulu na Mbarara .

Maandalizi ambayo yamefanyika ni kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, kuandaa watoa huduma wa afya kwa ajili ya msaada wa kisaikoloji na mafunzo ya namna ya kuzika watu kwa usalama na kwa hadhi.

Halikadhalika elimu kwa jamii na taarifa ambapo watu milioni mbili wamepokea taarifa kupitia mbinu mbali mbali zinazotumika ikiwemo mazungumzo ya uso kwa uso kutoka nyumba moja hadi nyingie katika wilaya za hatari ya juu. Aidha taarifa kupitia radio na televisheni, chapisho zinasambazwa na ujumbe.

Uganda imeweka mikakati katika maeneo ya mipakani ikiwemo kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe ambako wafanyakazi wamepokea namna ya kugundua mgonjwa.

Licha ya maandalizi yaliyopo wizara ya afya imesema bado kuna kazi inayohitaji kufanywa katika maeneo ya kukabiliana na taka na usimamizi katika vituo vidogo vya afya na upokezi wa wasafiri kutoka na kueleka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako kunashuhudiwa mlipuko wa ebola.

Baadhi ya mambo ambayo yametajwa kama muhimu katika kujiandaa kukabiliana na gonjwa hilo ni ushirikiano katika maeneo ya mipaka, ushiriki wa jamii na upanuzi wa shughuliza maandalizi katika wilaya zingine. Aidha chanjo dhidi ya ebola kwa wahudumu wa afya waliko mstari wa mbele.