Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akili Bandia tayari inaleta mapinduzi ya matibabu Tanzania

Pichani ni aina ya roboti inayotumia akili bandia kwa aiji  ya kusaidia mtoto ambaye amezaliwa na ugonjwa usio wa kawaida huko Ireland.
ITU/M.Jacobson-Gonzalez
Pichani ni aina ya roboti inayotumia akili bandia kwa aiji ya kusaidia mtoto ambaye amezaliwa na ugonjwa usio wa kawaida huko Ireland.

Akili Bandia tayari inaleta mapinduzi ya matibabu Tanzania

Afya

Mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu akili bandia, au AI ukiendelea huko Geneva, Uswisi, nchini Tanzania inaelezwa kuwa tayari akili bandia imeanza kutumika kuboresha huduma za afya hasa katika maeneo yenye uhaba wa daktari.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa Castory Munishi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba, Muhimbili, MUHAS nchini Tanzania, chuo ambacho hivi karibuni kiliendesha mdahalo kuhusu akili bandia na nafasi yake katika kuimarisha huduma za afya.

Akihojiwa kwa njia kutoka Dar es salaam Tanzania na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili  ya Umoja wa Mataifa, Munishi ametolea mfano daktari msaidizi, au Dokta Elsa akisema, « anatumika Arusha, yeye anatumiwana wasaidizi wa afya ambaye anawashauri. Mgonjwa akija wanaingiza dalili alizosema, kwa huyu daktari Elsa ambaye ni mfumo wa akili bandia anaweza kujifunza na kuzitafsiri taarifa alizopewa na mgonjwana kueleza mgonjwa ana ugua nini. »

Alipoulizwa Daktari Elsa amepata wapi ujuzi huo, Munishi amesema, « daktari Elsa alifundishwa kutokana na mafaili ya wagonjwa yaliyokuwepo hospitali kwa sababu  mifumo ya akili bandia kikubwa inayoifanya iweze kuwepo na kuwepo ni kufundishwa kutokanana data. »

Amesema kwa kufanya hivyo , « mtaalamu wa afya ambaye si daktari kutokana na upungufu wa madaktari,  anaingiza dalili alizosema mgonjwa na kwa kuwa Daktari Elsa ameshajifunza, mtu labda anaumwa kichwa, homa au anatapika anaweza kuwa anaugua Malaria, kwa hiyo anasema pengine mgonjwa anaugua ugonjwa fulani . »

Munishi amesema mtaalamu wa afya atajumuisha ufahamu wake na kile ambacho amesema Daktari Elsa kuhusu mgonjwa na kisha wanamfanyia matibabu na uhakika ni zaidi ya asilimia 90.