Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa akili bandia wakutana Geneva, kubonga bongo ili iwe na maslahi kwa wote

Baadhi ya teknolojia za akili bandia au Artificial Intelligence za roboti zikionyeshwa kwenye mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu akili bandia  ulioanza leo huko Geneva, Uswisi.
ITU Twitter
Baadhi ya teknolojia za akili bandia au Artificial Intelligence za roboti zikionyeshwa kwenye mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu akili bandia ulioanza leo huko Geneva, Uswisi.

Wataalamu wa akili bandia wakutana Geneva, kubonga bongo ili iwe na maslahi kwa wote

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hii leo huko mjini Geneva, Uswisi kumeanza mkutano wa siku nne ukilenga kusaka mbinu na mikakati ya kuhakikisha kuwa akili bandia au AI inakuwa na manufaa kwa kila mkazi wa dunia hii.

Ukiwa umeandaliwa na shirika la mawasiliano duniani, ITU kwa  ubia na taasisi 37 za Umoja wa Mataifa,  mkutano huo wa ngazi ya juu unataka kutumia ushawishi wa Umoja wa Mataifa katika kuleta pamoja wadau mbalimbali wa ubunifu na utumiaji wa akili bandia.

Miongoni  mwao ni wawakilishi kutoka mashirika ya Umoja wa MAtaifa, kampuni ongozi kwenye akili bandia na mashirika ya kiraia pamoja an wanazuoni kutoka vyuo vikuu zaidi ya 50.

Mathalani wanasaka kupata miradi ya AI yenye faida kwa jamii lakini pia akili bandia ambayo ni salama, jumuishi kwenye maendeleo na yenye kuweza kutumiwa na wengi iwe kwenye sekta ya afya, elimu, ustawi wa kijamii, na utafiti.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa ITU, Houlin Zhao amesema kuwa, asilimia 50 ya hataza zote za akili bandia zimesajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na wakati  huo huo suala la akili bandia linaibua hoja ya, faragha, uaminifu na utu wa binadamu na usawa. Halikadhalika inaleta changamoto kubwa kwenye ajira, silaha zinazojifyatua zenyewe kiasi kwamba kampuni zenyewe za teknolojia zimeibuka na mbinu za kuhakikisha teknolojia ya akili bandia inakuwa wajibifu.

Bwana Zhao amesema ni dhahiri shairi kuwa  hakuna taifa moja, jamii moja au kampuni moja inaweza kukabili hizo changamoto peke yake.

Amesema mwelekeo wa kuleta mabadiliko thabiti na akili bandia yenye maslahi kwa wote na salama inahitaji ushirikianowa kipekee baina ya serikali, wanazuoni na kampuni bila kusahau mashirika ya kiraia.

Kwa mantiki hiyo amesihi washiriki zaidi ya 2,000 kutoka mtaifa 120 washiriki kwa kina katika mkutano huo wa tatu wa kimataifa kuhusu akili bandia ili hatimaye iweze kuchagiza maendeleo endelevu duniani.