Mwelekeo sasa ni akili bandia kusaidia nyanja zote- WIPO

Ripoti mpya ya shirika la hakimiliki duniani, WIPO inathibitisha kuwa akili bandia haitasalia kwenye masuala ya kiufundi pekee bali teknolojia hiyo itasambaa katika nyanja zote zinazogusa maisha ya binadamu kila siku.
Ikiwa imezinduliwa leo huko Geneva, Uswisi, ripoti inasema kuwa makadirio hayo yanatokana na ongezeko la maombi ya hataza ya ubunifu kwenye sekta hiyo.
WIPO imetolea mfano tangu mwaka 2013, asilimia 50 ya hataza zote zilizoombwa zikidurusu akili ya binadamu kufanywa na mashine iwe ni kwenye sekta ya usafirishaji na huduma za afya, zimechapishwa, ikiwa ni zaidi ya 170,000.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Francis Gurry amesema utafiti wa akili bandia ulianza miaka ya 1950, “lakini kumekuwepo na ongezeko kubwa tangu mwaka 2013, kwa hiyo tunashughulika na kile kinachotokea sasa kwenye nyanja inayokua kwa kasi kubwa.”
Amesema mbinu inayotafitiwa zaidi ni ile ya matumizi ya akili bandia kwenye mashine ikiwemo ile ya abiria zaidi ya mmoja kutumia apu ya kuwawezesha kuunganishwa na gari moja ili kupungumza mizunguko ya safari.
Hata hivyo Bwana Gurry ametaja pia utafiti katika utambuzi wa sauti ya mtu akisema nao unashika kasi kubwa ikiwa na ongezeko la asilimia 175 kwenye maomb yake ya hataza kutoka mwaka 2013 hadi mwaka 2016.
Hata hivyo amesema licha ya ongezeko hilo la maombi ya hataza kwenye uguduzi wa masuala yanayohusu akili bandia, ni nchi mbili tu ambazo ni Marekani na China ndio zinaongoza kwa kuwasilisha maombi hayo.
Kampuni ya IBM yenye makao yake makuu nchini Marekani iliongoza kwa kwa na maombi 8,290 ikiuatiwa na Microsoft maombi 5,930.
Bwana Gurry alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo dunia inakuwa bora zaidi kwasababu ya teknolojia, amesema sayansi inayotumika kwenye nyanja hiyo bado haina muegemeo wowote.
Hata hivyo amehoji, “je akili bandia ni habari njema au mbaya? Teknolojia haina muegemeo wowote na inategemea unaitumia vipi. Hadi sasa iwapo utatumia akili bandia kutengeneza mifumo inayojitegemea ya silaha inayoweza kutuua sote, hiyo si habari njema unajua, lakini iwapo itatumika kuimarisha viashiria vya afya, uchunguzi kwenye afya na kwa malengo hayo basi hizo ni habari njema.”