Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shirika la mawasiliano duniani, ITU lazindua ripoti mpya kuhusu akili bandia (AI) katika utangazaji.

Wabobezi wa teknolojia kuhusu Akili Bandia, AI wanakutana Geneva, Uswisi kwa siku tatu kusaka mbinu bunifu za kutumia teknolojia hiyo kama roboti hiyo pichani  kwa maslahi ya kila mtu bila changamoto zozote.
ITU/D. Procofieff

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hii leo mkutano wa tatu wa kiamataifa kuhusu akili bandia ukiingia siku ya pili mjini Geneva Uswisi, shirika la mawasiliano duniani ITU limetoa ripoti mpya inayoeleza namna akili bandia (AI) inavyoweza kutumika wakati wa mchakato wa kutengeneza na kusambaza matangazo ya televisheni na redio.

Ripoti inazungumzia namna ambavyo hivi sasa akili bandia inatumika kuboresha mtiririko katika utengenezaji wa programu za utangazaji, uboreshaji wa sauti na tathimini ya ubora wa picha, kutumia kwa ufanisi wigo wa masafa katika usambazaji wa televisheni na redio na hivi karibuni kuzalisha vipindi vipya kwa kufufua taarifa za zamani na pia kulenga taarifa kwa ajili ya walengwa au mtu mmoja mmoja.

Kwa mfano, akili bandia inatumika kufukua maudhui kutoka katika hifadhi za nyaraka nyingi za kale, kuyaandaa maudhui kwa ajili ya kusambazwa kimataifa na kuzalisha huduma kama vile maelezo kwenye sauti, maelezo ya sauti, kuhamisha maandishi kwenda kwenye sauti na ishara, kwa haraka na kwa usahihi kuliko ambavyo ingefikiwa hapo awali.

Baadhi ya teknolojia za akili bandia au Artificial Intelligence za roboti zikionyeshwa kwenye mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu akili bandia  ulioanza leo huko Geneva, Uswisi.
ITU Twitter
Baadhi ya teknolojia za akili bandia au Artificial Intelligence za roboti zikionyeshwa kwenye mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu akili bandia ulioanza leo huko Geneva, Uswisi.

Katibu Mkuu wa shirika la mawasiliano duniani, ITU, Houlin Zhao anasema, “ITU inashirikiana na wadau kuunganisha nguvu ya akili bandia kuboresha maisha duniani kote na kutafuta suluhu za changamoto kubwa za ulimwengu. Hii inatusaidia kutambua matumizi ya akili bandia ambayo yanaweza kuharakisha maendeleo katika kuelekea kwenye Malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa. Hicho ndicho tunachokifanya wiki hii katika  mkutano huu wa ngazi ya juu kuhusu akili bandia. Bado kuna kazi kubwa ya kufanya inayohitajika kuhakikisha kuwa matumizi ya akili bandia katika utengenezaji programu na usambazaji maudhui ni kwa faida ya hadhira.”

Mkutano huo utakaodumu kwa siku nne, umeandaliwa na shirika la mawasiliano duniani, ITU kwa ubia na taasisi 37 za Umoja wa Mataifa, mkutano huo wa ngazi ya juu unataka kutumia ushawishi wa Umoja wa Mataifa katika kuleta pamoja wadau mbalimbali wa ubunifu na utumiaji wa akili bandia.