Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Algeria na Argentina zaupa kisogo ugonjwa wa malaria:WHO

Afisa wa utibabu  akiwa anajitayarisha kupa damu kuona kama ina malaria.
PAHO/WHO Photo
Afisa wa utibabu akiwa anajitayarisha kupa damu kuona kama ina malaria.

Algeria na Argentina zaupa kisogo ugonjwa wa malaria:WHO

Afya

Algeria na Argentina zimethibitishwa na kutambulika rasmi na shirika la afya ulimwengu WHO kuwa zimetokomeza malaria.

Taarifa iliyotolewa leo na WHO inasema cheti cha uthibitisho huo hutolewa kwa nchi ambayo imedhihirisha kwamba imekomesha maambukizi ya maradhi asilia katika eneo hilo na kuwa huru bila maradhi hayo kwa takribani miaka mitatu mlululizo.

Malaria ugonjwa unatokana na kuumwa na mbu umesalia kuwa ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa vifo duniani, ikikadiriwa kwamba kwa mwaka 2017 pekee kulikuwa na visa milioni 219 na vifo zaidi ya 400,000 vya malari, huku aslimia karibu 60 ya vifo hivyo ni vya watoto wa umri wa chini ya miaka 5.

Algeria ni nchi ya pili katika ukanda wa Afrika wa WHO kutambuliwa rasmi kama imetokomeza malaria baada ya Mauritius ambayo ilithibitishwa rasmi na WHO kutokomeza malaria 1973.

Kwa upande wake Argentina ni nchi ya pili katika ukanda wa Amerika kuthibitishwa kutokomeza ugonjwa huo hatari katika miaka 45, ikifuata nyayo ya Paraguay iliyotangazwa rasmi kufanya hivyo Juni 2018. Algeria iliripoti kisa cha mwisho cha malaria mwaka 2013 wakati nchini Argentina kilikuwa mwaka 2010.

Mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na mama yake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.
© UNICEF/UN066838/Hubbard
Mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na mama yake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.

Jitihada zilizofanyika

Kwa mataifa yote mawili Algeria na Argentina malaria ina historia  iliyodumu mamia ya miaka na vita dhidi ya ugonjwa huo havikuwa rahisi . Lakini katika muongo uliopia kuboreshwa kwa huduma za uchunguzi na vipimo kwa kila kisa cha malaria kulisaidia sana katika kudundua  haraka na mapema na kutibu visa hivyo.

Kimsingi na cha muhimu zaidi WHO inasema nchi hizo zilitoa huduma ya malaria bure ya upimaji na matibabu katika mipaka yake , zilihakikisha hakuna aliyesalia nyuma katika kupata huduma wanazohitaji kwa ajili ya kuzuia, kubaini na kutibu ugonjwa huo. Akizungumzia hatua hiyo kubwa mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhamon Ghebreyesus amesema “Algeriana Argentina zimetokomeza malaria , shukran kwa dhamira na jitihada za watu na viongozi wa nchi zote mbili. Mafanikio yao  ni mfano kwa nchi zingine kufanya kila ziwezalo kuutokomeza ugonjwa huu kabisa.”

Historia ya malaria Algeria

Daktari wa Kifaransa Charles Louis Alphonse Laveran aligundua vijidudu vya malaria nchini Algeria mwaka 1880. Na kufikia miaka ya 1960 malaria ikawa ni changamoto kubwa ya kiafya nchini humo ikiwa na visa 80,000 vinavyoripotiwa kila mwaka.

Hivyo mafanikio ya Algeria kutokomeza malaria yametokana kuwa na wahudumu wa afya waliopatiwa mafunzo bora, upimaji wa malaria, matibabu kupitia mpango wa huduma bure kwa wote na hatua za haraka kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo. Kwa pamoja sababu hizo zimeifanya nchi kufikia lengo la kutokuwa na kisa hata kimoja cha malaria.

Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa Algeria ndiko wadudu wa malaria walikobainika kwa mara ya kwanza kwa binadamu zaidi ya karne moja na nusu iliyopita  na hiyo ndio ilikuwa chachu ya kupambana na ugonjwa huo amesema Dkt. Matshidiso Moet mkurugenzi wa kanda ya afrika wa WHO.

Ameongeza kuwa “Sasa Algeria imelidhihirishia barala la Afrika kwamba malaria inaweza kutokomezwa kupitoa uongozi wa serikali, hatua madubbuti, uwekezaji za sayansi. Nchi zingine katika bara hilo zinaweza kuchukua uzowevu wao.”

Kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora ikiwemo vyandarua vyenye viuatilifu ni muarobaini wa kuondokana na malaria.
WHO
Kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora ikiwemo vyandarua vyenye viuatilifu ni muarobaini wa kuondokana na malaria.

Safari ya Argentina kutokomeza malaria

Katika miaka ya 1970 Argentina ilijipanga kutokomeza malaria na mtazamo muhimu iliouchukua ilijumuisha mafunzo kwa wahudumu wa afya kupulizia dawa majumbani , upimaji wa malaria na kukabiliana kwa kina na visa vya ugonjwa huo vilivyozuka katika jamii. Ushirikiano na nchi jirani pia ilikuwa muhimu sana kwa Argentina Kati ya mwaka 2000 na 2011 Argentina ilishirikiana kwa karibu na serikali ya Bolivia kupuliza dawa katika nyumba zaidi ya 22,000 katika maeneo ya mpakani na kufanya vipimo vya malaria kwa watu wengi.

Kwa mujibu wa Dkt. Carissa F. Etienne mkurugenzi wa EWHO kwa ajili ya mataifa ya Amerika kwenye ofisi ya kikanda “Argentina iliripoti kisa cha mwisho cha malaria mwaka 2010 na imedhihirisha azma yake ya kusalia bila kisa, mfumo imara wa afya, uwezo wa kupambana na malaria, vipimo, ufuatiliaji wa ugonjwa huo na ufadhi unaohitajika katika kuzuia kuzuka tena kwa ugonjwa huo. Nina uhakika kwamba Argentina itakuwa kama chachu na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ya amerika katika kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huu hatari wa Malaria katika miaka ijayo.”


Vyeti kwa nchi hizo mbili vimekabidhiwa na mkurugenzi mkuu wa WHO kwa wakwakilishi kutoka Algeria na argentina kandoni kwa kikao cha 72 cha baraza la afya duniani kinachoendelea mjini Geneva Uswis.