Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya ni moja ya changamoto kubwa zitakazoikumba dunia muongo ujao:WHO

Vifaa vya kisasa katika hospitali nchini Cambodia vinasaidia kuokoa maisha
World Bank/Chhor Sokunthea
Vifaa vya kisasa katika hospitali nchini Cambodia vinasaidia kuokoa maisha

Afya ni moja ya changamoto kubwa zitakazoikumba dunia muongo ujao:WHO

Afya

Shirika la afya duniani WHO leo limetoa orodha ya changamoto kubwa za dharura za afya zinatakzoikumba dunia katika muongo ujao ulioanza mwaka huu. 

Kwa mujibu wa shirika hilo orodha hiyo imeandaliwa na maoni ya wataalam kutoka kote duniani na inadhihirisha masuala yanayotia hofu ambayo viongozi wa dunia wanashindwa kuwekeza vya kutosha katika vipaumbele na mifumo muhimili ya afya.

WHO inasema hili linaweka uhai wa mamilioni ya watu, maisha yao na uchumi wao njiapanda."Hakuna hata moja kati ya haya ni rahisi kushughulikia, lakini yote yanawezekana kuyashughulikia. Afya ya umma kwa hakika ni chaguo la kisiasa”  limesisitiza shirika hilo.

Akihimiza umuhimu wa kufanya hivyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhanom Ghebreyesus amesema, "tunahitaji kutambua kwamba kuwekeza katika afyua ni kuwekeza katika mstakabali wetu. Nchi zinawekeza kiasi kikubwa katika kuwalinda watu wake dhidi ya mashambulizi ya kigaidi, lakini sio dhidi ya mashambulizi ya virusi, ambavyo vinaweza kuua zaidi na kusababisha athari kubwa zaidi za kiuchumi na kijamii. Maradhi yanaweza kuufanya uchumi na mataifa kusambaratisha uchumi, na hii ndio sababu suala la usalama wa afya haliwezi kuwa la wizara ya afya pekee.”

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa changamoto zote hizi kwenye orodha zinahitaji kuchukuliwa hatua mathubuti kutoka kila sekta sio tu sekta za afya.Tunakabiliwa na tishio kubwa la pamoja na tuna wajibu wa pamoja kuchukua hatua. Wakati ukomo wa ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu ukinyemelea haraka, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limehimiza kwamba miaka 10 ijayo ni lazima iwe muongo wa kuchukua hatua.”

Dkt. Tedross amesema hii inamaanisha kwamba kuchagiza ufadhili wa kitaifa ili kushughulikia mapengo katika mifumo ya kiafya na miundombinu ya afya, pamoja na kutoa msaada kwa nchi zisizojiweza. “Kuwekeza sasa kutaokoa maisha na fedha hapo baadaye. Gharama ya kutofanya chochote hatuwezi kuimudu, serikali, jamii na mashirika ya kimataifa lazima yafanye kazi pamoja kutimia malengo haya muhimu. Hakuna njia ya mkato ya kuwa na dunia yenye afya, Mwaka 2030 unakaribia kwa haraka na ni lazima tuhakikishe viongozi wetu tunawawajibisha kwa ahadi zao.”