Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna bidhaa duniani yenye thamani zaidi ya afya:WHO

Mama Bendu akipokea mwanae waliyezaliwa kutoka kwa mkunga kituo cha Sinje nchini Liberia.
UNFPA/Elena Heatherwick
Mama Bendu akipokea mwanae waliyezaliwa kutoka kwa mkunga kituo cha Sinje nchini Liberia.

Hakuna bidhaa duniani yenye thamani zaidi ya afya:WHO

Afya

Wakati dunia hivi sasa ikikabiliwa na changamoto chungu nzima zinazoongeza mzigo katika huduma za afya, iwe vita, majanga ya asili, mabadiliko ya tabia nchi na hata milipuko ya magonjwa hakuna kilicho muhimu kama kuwa na afya njema.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, Dr. Tedross Adhamo Ghebreyesus wakati akifungua baraza kuu la 70 la afya dunia hii leo mjini Geneva Uswisi, na kuongeza kwamba,  “hakuna bidhaa yoyote iliyo na thamani zaidi afya, ni taasisi iliyo na jukumu la kuteteta afya ya watu bilioni 7, hivyo inabeba jukumu kubwa na ni lazima iwe katika kiwango cha juu.”

Amesema na kumbusho kubwa la wajibu huo ni pale panapojitokeza milipuko ya magonjwa na kudhihirisha umuhimu wa watu ambao WHO inawahudumia.

Amesema amefurahishwa na ari na kujitoa kwa wahudumu wa afya wa shirika hilo ambao kila uchao wanaweka maisha yao hatarini ili kuokoa ya wengine. La msingi ni kujiandaa akitolea mfano mlipuko wa Ebola unaoendelea hivi sasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC  akisema ingawa mlipuko umeingia mjini lakini maandalizi ya kuukabili ni mazuri kuliko ilivyokuwa 2014.

(Picha:UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi)
Ebola!

Naye Dkt. Peter Salama, Naibu Mkurugenzi  Mkuu wa WHO masuala ya dharura WHO akifafanua kuhusu kuanza leo kwa chanjo ya mzunguko ya Ebola ambayo  bado iko kwenye majaribio, iitwayo Zaire Ebola virus na ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa huko Guinea amesema, “Inaitwa chanjo kwa mfumo wa mzunguko kwa sababu hii si kampeni ya kawaida ya chanjo ambayo unapatia chanjo wakazi wote wa eneo fulani.Hii ina walengwa.Kimsingi unabaini mgonjwa, halafu unabaini watu wote waliokuwa karibu na mgonjwa huyo, na wengine waliokuwa karibu na hao, wakiwemo wahudumu wa afya na hiyo inakupatia mzunguko uliomzigira mgonjwa.”

Na kwa mantiki hiyo Dkt. Ghebreyesus amehimiza “Ni lazima tuchukue hatua za haraka kwa kila tunalolifanya , kwa sababu kila wakati tunaoupoteza ni suala la baina ya uhai au kifo.”  Ndio maana WHO inashirikiana na wadau kukomesha kifua kikuu au TB, imeanzisha miradi mipya kutokomeza malaria, imezindua mikakati ya kutokomeza utipwatiwa na mikakati mingine mingi kuhakikisha malengo ya afya yanatimia ifikapo 2030.

Kwa mantiki hiyo  WHO imeharakisha kuanzisha mkakati wa 13 wa kazi zake ujulikanao kama GPW, lengo likiwa kuchagiza afya bora, kuifanya dunia kuwa salama na kuhudumia wasiojiweza kwani, hatutoikubali dunia ambayo watu wanaugua kwa sababu ya hewa wanayovuta haifai kwa maisha ya binadamu, hatutoikubali dunia ambayo watu wanapaswa kuchagua baina ya ugonjwa na umasikini kwa sbabu gharama za kulipia huduma kutoka mifukoni mwao.”

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
UN/Daniel Johnson
Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus

Na ili hili lifanikiwe amesema kuna masula matatu ya kuzingatia, mosi ni kuwa na shirika la WHO lililo imara na linaloleta mabadiliko, pili kuwa na mkakati wa kuleta mabadiliko kulifanya shirika hilo kufanya kazi vizuri na kuzaa matunda na tatu lakini pia kuhakikisha suala la jinsia linapewa uzito mkubwa.

Baraza hilo kuu la afya duniani limewaleta pamoja nchi wanachama, wataalamu , wadau wa afya na wanaharakati kutoka kote duniani na litakunja jamvi  tareje 26 mwezi huu wa Mei.