Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza Malaria kunaanza na mimi- WHO

Mlinda amani wanayehudumu nchini Sudan Kusini akihudumia mwanamke mjamzito anayeugua malaria.Watoa huduma wakati mwingi ni walengwa wa mashamubulio
UNMISS
Mlinda amani wanayehudumu nchini Sudan Kusini akihudumia mwanamke mjamzito anayeugua malaria.Watoa huduma wakati mwingi ni walengwa wa mashamubulio

Kutokomeza Malaria kunaanza na mimi- WHO

Afya

Leo ni siku ya malaria duniani na shirika la afya ulimwenguni WHO limeungana na nchi na wadau wengine kote duniani kuhimiza vita dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria likimtaka kila mmoja kushiriki vita hivyo ili kufikia ajenda afya ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030. 

Ujumbe huo wa WHO ni mahsusi kwa ajili ya siku hii ambayo  kila mwaka huadhimishwa Aprili 25, na mwaka huu imebeba kauli mbiu ya kutokomeza malaria isemayo “Kutokomeza Malaria kunaanza na mimi.”

Kwa mujibu wa shirika hilo japo kuna hatua zilizopigwa katika vita dhidi ya malaria lakini sio kubwa sana katika kupunguza visa vya malaria kati ya mwaka 2015 na 2017, huku vifo vilivyotokana na malaria kwa mwaka 2017 vikiwa 435,000 duniani kote idadi ambayo haijabadilika sana ikilinganishwa na miaka iliyopita na watu milioni 250 wanakumbwa na ugonjwa huo kila mwaka..

Sasa WHO inasema hatua za haraka zinahitajika kote duniani ili kurudisha vita dhidi ya malaria katika msitari unaotakiwa zikishirikisha wadau wote zikiwemo jamii na wanajamii. Akihimiza vita hivyo katika ujumbe wake maalumu wa siku hii mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamo Ghebreyesus amesema, “athari zake zinakwenda mbali zaidi katika maisha , malaria inabebesha  mzigo mkubwa mifumo ya afya, inasitisha uzalishaji na inadumaza ukuaji wa uchumi.”

Mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na mama yake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.
© UNICEF/UN066838/Hubbard
Mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na mama yake baada ya kupewa dawa ya kutibu malaria katika zahanati ya kijiji katika wilaya ya Kasungu Malawi.

 Na kisha anahimiza wadau akisema kwamba,  ""tunatoa wito kwa viongozi wa siasa, sekta binafsi na jamii zilizoathirika kuchukua hatua kuboresha uzuiaji, upimaji na tiba ya malaria.Wote tuna jukumu la kufanya. Kuwekeza katika huduma ya afya kwa wote ni njia bora ya kuhakikisha kwamba jamii zote zina fursa ya huduma zinazohitaji kutokomeza malaria na magonjwa mengine. Siku hii ya Malaria duniani ungana nasi kutangaza kwamba kutokomeza malaria kunaanza na mimi.”

Kampeni maalum ya kutokomeza malaria kunaanza na mimi ambayo inaanzia mashinani  inaendeshwa na WHO ikishirikiana na wadau wengine ukiwemo mradi wa RBM  wa kutokomeza malaria, Tume ya Muungano wa Afrika, mpango wa Rollback Malaria na wadau wengine kwa lengo la kuhakikisha ugonjwa huo hatari unasalia kileleni kwenye ajenda za kisiasa , lakini pia kukusanya rasilimali  zinazohitajika katika vita hivi na kuziwezesha jamii jamii kuchukua usukani wa malaria katika kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huo.