Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunajiandaa kukabiliana na kimbunga Fani Bangladesh:UN

Msichana mkimbizi akiwa amesimama nje kwenye mvua katika kambi ya Shamlapur, Cox's Bazaar
UNHCR/Patrick Brown
Msichana mkimbizi akiwa amesimama nje kwenye mvua katika kambi ya Shamlapur, Cox's Bazaar

Tunajiandaa kukabiliana na kimbunga Fani Bangladesh:UN

Tabianchi na mazingira

Kimbunga kikali Fani kinachoambatana na mvua kubwa na upepo mkali kimeikumba India katika eneo la Puri  mjini Odisha leo limesema shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO.

Kimbunga hicho kikiwa na upepo wa kasi ya kilometa 180-190 kwa saa kinatarajiwa pia kuelekea katika eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo na kisha kwenda Magharibi mwa Bengali na nchini Bangladesh.

WMO inasema idara ya kudhibiti majanga ya India imekuwa na maandalizi makubwa kukabiliana na kimbunga hicho na imeshahamisha watu milioni moja na kuwashauri wengine nini cha kufanya lakini pia kutoa tahadhari ikiwemo pia kufunga shule na viwanja vya ndege.

Kwa upande wa Bangladesh mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa likiwemo la mpango wa chakula WFP yanaendelea na maandalizi katika eneo la Cox's Bazaar nchini Bangladesh ili kukabiliana na athari zozote zitakazosababishwa na kimbunga Fani kwa wakimbizi.

Akizungumzia maandalizi hayo msemaji wa WFP Herve Verhoosel amesema “Wafanyakazi wa WFP mjini Cox’s Bazar hivi sasa wanaendelea kufuatilia kwa aribu kimbunga Fani hasa athari zake katika makambi ya wakimbizi. Kuna akiba ya ziada ya msaada wa chakula na kingine cha dharura endapo kutakuwa na athari zozote.”

WFP imekamilisha kazi ya tathimini ya uhandisi na kupunguza hatari ya majanga ili kuhakikisha makambi ya wakimbizi ni salama na yanafikika kwa urahisi wakati wa msimu wa mvua za Monsoon na vimbunga.

Umoja wa Mataifa unasema timu zake tayari ziko huko zikiendelea na maandalizi wakati kimbunga hicho Fani kikitarajiwa kuwasili Bangladesh mwishini mwa wiki hii na huenda kuathiri makambi ya wakimbizi.