Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wakihaha kuwafikia manusura Pemba, WFP yaanza kusambaza chakula kwa helikopta hii leo

Wafanyakazi wa misaada kutoka Mission Aviation Fellowship, MAF, wakipakua vifaa vya matibabu vilivyowasilishwa na UNICEF hii leo tarehe 30 Aprili 2019
UNICEF/DE WET
Wafanyakazi wa misaada kutoka Mission Aviation Fellowship, MAF, wakipakua vifaa vya matibabu vilivyowasilishwa na UNICEF hii leo tarehe 30 Aprili 2019

Wahudumu wakihaha kuwafikia manusura Pemba, WFP yaanza kusambaza chakula kwa helikopta hii leo

Msaada wa Kibinadamu

Wahudumu wa misaada ya kibinadamu wamekuwa wakikimbizana kuwafikishia waathirika wa kimbunga Kenneth msaada wa dharura baada ya mvua kusita kwa muda leo asubuhi mjini Pemba nchini Msumbiji.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya binadamu OCHA miongoni mwa hatua zinazochukuliwa kufikisha msaada haraka ni kwa kutumia ndege kupeleka mahitaji ya muhimu ikiwemo vifaa vya tiba katika kisiwa cha Matemo moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na kimbunga hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema,  "timu ya wafanyakazi wa dharura pia watafanya tathini ya uharibifu na mahitaji zaidi kadri watakavyoweza , wakati mvua zaidi zikitarajiwa katika siku zijazo na hivyo kufanya operesheni kuuendelea na zikisimama. Msumbiji kimbunga kimesambaratisha kabisa au kuharibu Karibu nyumba 35,000 na madarasa 200, kuwaacha maelfu ya watu bila makazi na watoto bila kwenda shule. Pia vituo vya afya 14 vimeathirika.”

Kwa mujibu wa duru za serikali watu 38 wamefariki duniani nchini Msumbiji na wanne nchini Comoro kufuatia kimbunga Kenneth. Hivi sasa watu 21,000 wanahifadhiwa katika vituo baada ya vijiji vyao kusambaratishwa kabisa huku wahudumu wa OCHA waliofanya tathimini kwa njia ya anga wakisema baadhi ya vijiji vinaonekama kama vimebomolewa na tingatinga.

Katika kusaidia mahitaji ya dharura mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF jana umetoa tena dola milioni 13, ambazo milioni 10 ni kwa ajili ya Msumbiji na milioni 3 kwa ajili ya Comoro. 

Umoja wa Mataifa pia umewashukuru wahisani kwa misaada yao hadi sasa ingawa unasema ombi la dola milioni 337 kwa ajili ya kukabiliana na athari ya vimbunga vyote viwili limefadhiliwa chini ya asilimia 30.

Makazi yamesambaratishwa huko wilaya ya Macomia jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji kufuatia kimbunga Kenneth kupiga eneo hili wiki iliyopita.
OCHA/Saviano Abreu
Makazi yamesambaratishwa huko wilaya ya Macomia jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji kufuatia kimbunga Kenneth kupiga eneo hili wiki iliyopita.

Helikopta za WFP zaanza kusambaza chakula kwa helikopta Cabo Delgado hii leo

Helikopta za shirika la mpango wa chakula duniani, WFP zimeanza hii leo kusambaza misaada ya chakula kwa waathiriwa wa kimbunga Kenneth kilichopiga eneo la Pemba jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji wiki iliyopita.

Msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi, Hervé Verhoosel amewaambia waandishi wa habari kuwa helikopta ya  kwanza imeondoka eneo la Quissanga ikiwa na tani 2.8 za biskuti zenye virutubisho pamojana tani moja ya chakula na kilo 100 za vifaa vya huduma za afya na dharura.

Amesema timu za uokoaji kutoka Afrika Kusini zinasaidia usambazaji wa chakula kwenye visiwa vya Ibo, Matemo na Quirimba .

Bwana Verhoosel amesema kisiwa cha Ibo kimeathirika zaidi kwa kuwa taswira kutoka angani inaonyesha kuwa kuwa nyumba zote zimebomolewa, wakazi wamepoteza akiba ya chakula na hivyo misaada zaidi ya chakula, malazi na huduma za kujisafi inahitajika.

Kama hiyo  haitoshi, wakazi wa maeneo hayo wamepoteza mbinu zao za kujipatia kipato na kwa kuzingatia kuwa kimbunga Kenneth kimepiga wakati wa kilele cha msimu wa mavuno hivyo hali ya upatikanaji wa chakula kwa kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu unatia mashaka.

WFP imesema inahitaji fedha za nyongeza ili kuhakikisha inaweza kusaidia taifa hilo la Msumbiji kujikwamua kutokana na athari za vimbunga Kenneth na Idai.

Tangu kimbunga Kenneth kipige jimbo la Cabo Delgado wiki iliyopita, WFP imeshafikishia msaada wa chakula watu 11,500 na sasa inahaha kuhakikisha kuwa inaweza kutoa msaada kwa kipindi cha miezi mitatu.