Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa wananchi wa kawaida vitendo ni bora kuliko maneno au hotuba:Espinosa

María Fernanda Espinosa Garcés;Rais wa kikao cha 73 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , akizungumza wakati wa ufunguzi wa mjadala wa wazi wa Baraza hilo
Picha na UN/Cia Pak
María Fernanda Espinosa Garcés;Rais wa kikao cha 73 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , akizungumza wakati wa ufunguzi wa mjadala wa wazi wa Baraza hilo

Kwa wananchi wa kawaida vitendo ni bora kuliko maneno au hotuba:Espinosa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Maneno matupu na hotuba bila vitendo halisi na hatua zinazoonekana katika kusongesha ajenda ya maendeleo endelevu, havina faida yoyote kwa mwananchi wa kawaida. Hayo yamesemwa leo na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati wa ufunguzi wa hafla ya maadhimisho ya kwanza ya siku ya ushirikiano wa kimataifa na amani kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New york Marekani.

Rais wa Baraza Kuu  la Umoja wa Mataifa Maria Fernando Espinosa akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya kwanza kabisa ya "siku ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani" amesema jumuiya ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa unahitaji kuongeza juhudi zake mara mbili kuhakikisha jamii, makundi yaliyotengwa, masikini wa kupindukia na wasio na sauti hawaachwi nyuma katika nyanja zote ikiwemo maendeleo, amani, haki za binadamu, mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia,  elimu na masuala mengine muhimu kwa ajili ya mustakbali wao.

Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa ina wajibu na fursa ya kutekeleza hayo. Na kwa upande wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba juhudi za kupata matokeo bora zaidi ya ajenda mbalimbali za Umoja wa Mataifa ni lazima tuwe na shirika ambalo linawajibika vyema, lililo na uwazi zaidi, lenye mshikamano na linalokidhi maratajio ya watu.

Na katika utekelezaji wa ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs, Bi. Espinosa amesema “endapo tutapiga hatua zinazoonekana katika mchakato wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, hali hiyo halisi kwa watu walioko mashinani itaboresha maisha ya kila mmoja wao na ukweli huo halisi utakuwa na nguvu zaidi ya hotuba yoyote tutakayoitoa hapa katika jukwaa hili. Hebu tuwe na ujasiri  na dhamira ya kubadili na kuboresha mbinu za utendaji kazi wetu, ubora wa masuluhisho tunayoamua na bila shaka pia utekelezaji wake.”

Amehimiza kuwa wakati wa kutekeleza yote hayo ni sasa, na ni kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Siku hii ya “ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani” imeadhimishwa baada ya azilio lililopitishwa na Baraza Kuu tarehe 18 Disemba 2018 na kuamua kwamba kuanzia sasa siku hii itaadhimishwa kila mwaka tarehe 24 Aprili .