Akiwa Urusi Guterres aonya dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kudorora kwa uchumi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameainisha changamoto za utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDG’s na kukumbusha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kwenye jukwaa la kimataifa la kiuchumi 2019 (SPIEF) linalofanyika huko St. Petersburg nchini Urusi.
Akizungumza katika jukwaa hilo Guterres amesema anaamini utandawazi na maendeleo ya teknolojia katika muongo uliopita vimechangia kwa kiasi kikubwa katika utajiri wa dunia.
Hata hivyo ameonya kwamba “utandawazi huohuo na maendeleo hayohyo ya teknolojia vimeongeza kwa kiasi kikubwa pengo la kutokuwepo kwa usawa duniani na kuwaacha watu, kanda, sekata na maeneo mengine nyuma.”
Agenda ya 2030
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres ukweli huu ulio bayana unatengeneza tofauti ambazo matokeo yake zinasababisha pengo kubwa la kutoaminiana baina ya watu, taasisi za kisiasa na mashirika ya kimataifa.
Wawakilishi katika jukwaa hilo la kimataifa la uchumi wameeleza kwamba Umoja wa Mataifa na nachi wanachama wameelezea ajenda ya 2030 ambayo inadhamiria kutumia fursa ya marendeleo ya teknolojia na utandawazi kutokomeza umasikini, kukomesha njaa, kuendeleza elimu, afya na hata mazingira miongoni mwa mengi.
Katibu Mkuu anatambua kwamba kuna malengo mengi makubwa na muhimu na kwamba kuna ucheleweshaji katika kuyatimiza. Kandoni mwa jukwaa hilo la kiuchumi la kimataifa kwa mwaka 2019 amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov na kujadili masuala mbalimbali.
Teknoloji
Kwa Guterres kudorora kwa uchumi ni moja ya vikwazo vikubwa vya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDG’s akieleza kwamba “vita vya biashara na migogoro inayohusiana na masuala ya teknolojia vinachangia hali tete na kuyumba kwa masoko.” zaidi ya hayo kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema “mabadiliko ya tabianchi ni changamoto nyingine kubwa inayotukabili sote. Teknolojia mpya iitwayo mapinduzi ya nne ya viwandani tishio lingine hususan katika soko la ajira , utabiri ni kwamba kutakuwa na umuhimu mkubwa wa kuunda ajira moja na kusambaratisha kwa kiasi kikubwa zingine, ni lazima kufikiria upya mifumo ya elimu.”
Kuhusu China
Alipoulizwa na mshiriki endapo ni muhimu zaidi kuwaodoa watu kutoka kwenye umasikini au kuchagiza haki za binadamu , Guterres amesemba kwamba “kuwaondoa watu katika umasikini ni haki ya msingi ya binadamu”. Akikumbusha kwamba misingi hii ni zaidi ya haki za kisiasa na kijamii huku akisisitiza kwamba mafanikio makubwa ya kuwaodoa watu katika umasikini duniani yamefanywa na Uchina katika miongo kadhaa iliyopita. Pia amezungumzia mpango wa serikali ya China wa kutokomeza kabisa umasikini nchini mwake ifikapo mwaka 2020, ingawa pia amesema hakubaliani na baadhi ya masuala ya haki za binadamu nchini humo.
Ushirikiano wa kimataifa
Katika hotuba yake Katibu mkuu pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa huku akipinga mtazamo kwamba ushirikiano wa kimataifa umesalia kuwa ni “mgongano baina ya Marekani na Uchina au vita baridi baina ya Marekani na Uchina.”
Kwa Guterres ni muhimu sana kwa dunia ya sasa ambapo Marekani, Uchina, Shirikisho la Urusi, India, Muungano wa Ulaya na wadau wengine muhimu kuweza kutatua matatizo yao kwa njia za ushirikiano wa kimataifa kwani pande zote hizo zina jukumu kubwa katika masuala ya kimataifa.