Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bodi ya ushauri ya UN na njia mpya ya kufikia utawala bora wa kimataifa 

Wanawake nchini Tanzania wakivuna seaweed kama sehemu ya mradi wa kilimo bora cha hali ya hewa.
UN Women/Phil Kabuje
Wanawake nchini Tanzania wakivuna seaweed kama sehemu ya mradi wa kilimo bora cha hali ya hewa.

Bodi ya ushauri ya UN na njia mpya ya kufikia utawala bora wa kimataifa 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuna haja ya kuwa na mabadiliko makubwa katika utawala wa kimataifa ili kukabiliana vyema na changamoto za sasa na zinazokuja kama janga la tabianchi na kuongezeka kwa vitisho vya usalama, kulingana na ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa leo Jumanne. 

Ripoti hiyo iliyozinduliwa na Bodi ya Ushauri ya Ngazi ya Juu ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ushirikiano wa Kimataifa wenye Ufanisi, Mafanikio kwa Watu na Sayari: Utawala Bora na Shirikishi wa Ulimwengu wa Leo na Wakati Ujao, inaeleza mpango kabambe wa kurekebisha usanifu wa kimataifa. 

Wakiongozwa na Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, na Waziri Mkuu wa zamani wa Uswisi, Stefan Löfven, Bodi ya Ushauri iliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres mnamo mwaka 2022, na ikapewa jukumu la kuzishauri Nchi Wanachama kuhusu masuala muhimu ya kimataifa ambapo utawala bora unaweza kuleta mabadiliko. 

Hukumu ya baadaye 

"Vizazi vijavyo vitatuhukumu kwa maamuzi tunayochukua leo," Bwana Löfven amesema. 

"Ushirikiano wa kimataifa unaweza kufanya kazi, lakini lazima ufanye kazi vizuri zaidi na haraka," ameongeza. "Mapendekezo yetu yanayohusu watu yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuunga mkono utekelezaji wa haraka wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Mkataba wa Paris [kuhusu mabadiliko ya tabianchi]." 

Bi Johnson Sirleaf amekubaliana na hilo akisema, "Nina imani kwamba ripoti inatoa mfumo ambao Umoja wa Mataifa, Nchi Wanachama, na wengine wanahitaji kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kizazi cha sasa na kijacho," amesema, akibainisha kuwa ripoti hiyo imekana na ushirikiano wa mwaka mzima wa ushirikishaji mamia ya mashirika, mitandao, na makundi mbalimbali ya asasi za kiraia yaliyojitolea kushughulikia changamoto za kimataifa. 

"Majibu waliyoleta yatasaidia vizazi vya sasa na vijavyo kuzuia athari mbaya za mwelekeo wetu wa sasa na kupata ulimwengu endelevu zaidi, wa haki na wa amani kwa watu na sayari dunia," ameeleza Bi Sirleaf. 

Usanifu wa kimataifa wenye nguvu zaidi 

Mapendekezo hayo yanajumuisha kuimarisha usanifu wa kimataifa wa amani, usalama na fedha, kufanikisha mabadiliko ya haki ya hali ya tabianchi  na uwekaji digitali, na kuhakikisha usawa zaidi na usawa katika kufanya maamuzi duniani. 

Ripoti hiyo pia inasema kuwa usawa wa kijinsia unahitaji kuwa kiini cha mfumo wa kimataifa ulioimarishwa upya pamoja na mapendekezo ili kuhakikisha kuwa mfumo unakuwa wa mtandao zaidi, unaojumuisha zaidi, na ufanisi zaidi.