Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kliniki  ya macho Beni nchini DRC yasaidia manusura wa Ebola

Manusura wa Ebola akifanyiwa uchunguzi wa macho kwenye kliniki huko Beni, Jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
J.D.Kannah/WHO
Manusura wa Ebola akifanyiwa uchunguzi wa macho kwenye kliniki huko Beni, Jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Kliniki  ya macho Beni nchini DRC yasaidia manusura wa Ebola

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Congo, DRC shirika la afya ulimwenguni WHO kwa kushirikiana na Wizara ya afya pamoja na vyuo vikuu viwili kutoka Marekani wanasaidia manusura wa Ebola kujiepusha na ugonjwa wa macho.

Shirika la afya ulimwenguni WHO linasema manusura hao huko kwenye jimbo la Kivu Kaskazini wanakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo uoni hafifu utokanao na kuwepo kwa uvimbeuchungu ndani  kwenye macho.

Ili kukabiliana na matatizo kama hayo, Wizara ya Afya na WHO walianzisha kliniki ya macho kwenye mji wa Beni ambao ni kitovu cha mlipuko wa sasa wa Ebola ulioanza mwezi Agosti mwaka jana, kliniki ikiwa na vifaa vya kisasa zaidi.

Kliniki hii ya macho ni nyongeza ya kliniki zinazoendeshwa kwa mwezi mara moja kwa ajili ya manusura wa Ebola kwenye mji huo wa Beni pamoja na ile ya Mangina na Butembo tangu mwezi Novemba mwaka jana.

Dokta Jessica Shantha kutoka Chuo Kikuu Emory nchini Marekani anasema, “tunawachunguza wagonjwa mapema zaidi kuliko tulivyofanya awali. Inawezekana kuwa hawajapata huu ugonjwa. Kwa hiyo ni jambo ambalo wanapaswa kufuatiliwa kwa muda mrefu ili kuhakiisha hawapati tatizo au uvimbeuchungu kwenye macho. Na pia nadhani sote bado tunajifunza kutoka kwa manusura wa Ebola, ugonjwa wa macho na matatizo ya macho.”

Dkt. Jessica Shantha (kushoto) na Dkt. Steven Yeh (Kulia) maprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani wakichunguza macho ya manusura wa Ebola kwenye kliniki iliyoanzishwa huko Beni, Kivu Kaskazini nchini DRC.
J.D.Kannah/WHO
Dkt. Jessica Shantha (kushoto) na Dkt. Steven Yeh (Kulia) maprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani wakichunguza macho ya manusura wa Ebola kwenye kliniki iliyoanzishwa huko Beni, Kivu Kaskazini nchini DRC.

Ufahamu uliopatikana kufuatia mlipuko wa Ebola ukanda wa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 hadi 2016 uliibua changamoto lukuki zinazokumba manusura wa Ebola ikiwemo uoni hafifu usababishwao na uvimbeuchungu machoni.

WHO inasema kwa kubaini na kutibu magonjwa hayo mapema, “unakuwa umepunguza madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea ikiwemo kutokuona kabisa. Mabingwa wa kimataifa wa magonjwa ya macho sasa wanawafundisha madaktari wa macho nchini DRC jinsi ya kubaini na kutibu magonjwa hayo na wataendelea kufuatilia wagonjwa.

Dkt. Telesphore Mumbere ni miongoni mwa madaktari hao na anasema, “kwa ushirikiano na WHO tunapaswa kuwaona hawa wagonjwa kila mwezi ili kutathmini waliopatiwa tiba kama wanapata nafuu na kwa wengine kuona iwapo wamepata tatizo zaidi kama ambavyo tumeshuhudia leo hii.”

Catherine ni miongoni mwa wanufaika wa  huduma ya matibabu ya macho. Baada ya kuruhusiwa kuondoka kituo cha matibabu ya Ebola huko Beni mwezi Oktoba mwaka 2018, Catherine akiwa naye hatarini kupata ugonjwa wa macho, alifika kituo na kupata huduma na anasema kuwa, “niliweza kuona kuwa walikuwepo pale kutupatia matibabu. Sikuhofia, nilielewa kuwa wanatibu macho yetu. Walikuwepo watu wengi wakiwemo wazungu.”

Hivi sasa kuna manusura zaidi ya 300 wa Ebola ambao wamejisajili kupata matibabu ya macho.