Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama wahitajika ili harakati dhidi ya Ebola DRC zifanikiwe- WHO

Chanjo dhidi ya Ebola kwanza kwa wahudumu wa afya imeanza Mashariki mwa DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
WHO-Eugene Kabambi
Chanjo dhidi ya Ebola kwanza kwa wahudumu wa afya imeanza Mashariki mwa DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Usalama wahitajika ili harakati dhidi ya Ebola DRC zifanikiwe- WHO

Afya

Viongozi waandamizi wa shirika la Afya duniani , WHO wameshuhudia matatizo yaliyopo katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Taarifa ya WHO iliyotolewa mjini Beni nchini DRC na Brazzaville Jamhuri ya Congo imetaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na watoa huduma kushindwa kufika kwa eneo la Mangina  lililoko umbali wa kilomita 30 kutoka Beni, ambalo ndilo  kitovu cha mlipuko wa sasa na kuna wagonjwa wengi.

 

Dawa dhidi ya Ebola nchini DRC likipakuliwa kutoka kwa ndege Mavivi katika Kivu Kaskazini August 2018
MONUSCO-AVIATION
Dawa dhidi ya Ebola nchini DRC likipakuliwa kutoka kwa ndege Mavivi katika Kivu Kaskazini August 2018

 

Eneo hili lina makundi mengi yenye silaha na kwa hivyo hali ya usalama si nzuri na imeleta changamoto kubwa kwa timu za maafisa wa afya  wanaotaka kuingia ndani mwa vijiji kufanya kazi za kukutana na jamii na pia kuchunguza hali ya kiafya mara tatu kwa kipindi cha wiki tatu.

Wakizungumza baada ya ziara yao, viongozi hao Dkt. Tedros Ghebreyesus ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa WHO pamoja na na mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti wametaka hatua zaidi ili watoa huduma waweze kufanya kazi zao.

Dkt. Tedros amesema, “WHO inatoa wito  kwa wahusika kutoa nafasi ya mazingira huru na salama kwa watu wa maeneo yaliyoathirika.”

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
UN/Daniel Johnson
Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus

 

 Ameongeza kuwa , “ wale wote wanaoshiriki katika harakati za kushughulikia mlipuko huo wanapaswa  kutembea kwa  uhuru na kwa usalama katika maeneo hayo ili waweze kufanya kazi yao inavyohitajika kuweza kudhibiti mlipuko huo .

Halikadhalika amesema wananchi ni lazima waweze kufikia vituo vya matibabu ambavyo vinaokoa maisha na kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.

Naye Dkt Moeti amesema kuwa ,”WHO ina uzoefu mkubwa  wa kutoa huduma za kiafya katika maeneo yenye migogoro barani Afrika , tutatumia uzoefu huu kuona kuwa wafanyakazi  pamoja na washirika wetu watafanya kila wawezalo kuweza kuokoa maisha ya watu wanaohitaji msaada.”

 

Mkurugenzi wa kanda ya Afrik ya WHO,Dkt Matshidiso Moeti (wapili kutohoto) akiwa Kinshasa DRC kuhusu mbinu za kukabilian dhidi ya Ebola
Photo: WHO
Mkurugenzi wa kanda ya Afrik ya WHO,Dkt Matshidiso Moeti (wapili kutohoto) akiwa Kinshasa DRC kuhusu mbinu za kukabilian dhidi ya Ebola

 

Ujumbe huo wa WHO ukiongozana na Waziri wa Afya wa DRC, Dkt. Ply Ilunga, umeshuhudia uzinduzi wa kuwapa chanjo wafanya kazi wa huduma ya kiafya katika  hospitali ya rufaa ya mjini Beni.

Pia wametembelea kituo cha dharura mjini Beni ambacho kilijengwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC- MONUSCO na baadaye kukikabidhi kwa washirika wao.

Licha ya kuwa huu ni mlipuko wa 10 wa Ebola lakini hii ni mara ya kwanza mlipuko unatokea katika eneo lenye watu wengi tena lenye mgogoro wa kivita, imesema taarifa hiyo.