Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya ebola vyapungua Beni, lakini tusibweteke- WHO

Juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa DRC ni za pamoja. Hapa MONUSCO na UNPOL wakitoa vifaa vya kutumiwa kama vile hema, viti na vinginevyo kwa mkuu wa Polisi ya Beni kutumiwa kwa kazi hiyo.
MONUSCO / Gweny Angel Nouko
Juhudi za kukabiliana na Ebola Mashariki mwa DRC ni za pamoja. Hapa MONUSCO na UNPOL wakitoa vifaa vya kutumiwa kama vile hema, viti na vinginevyo kwa mkuu wa Polisi ya Beni kutumiwa kwa kazi hiyo.

Visa vya ebola vyapungua Beni, lakini tusibweteke- WHO

Afya

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, visa vya ebola katika kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini vimeripotiwa kupungua. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linasema kuwa kupungua kwa visa vya ebola kwenye eneo hilo la Beni ambalo lilikuwa kitovu cha mlipuko wa mwaka jana wa ebola, ni dalili njema kuwa harakati za kudhibiti ugonjwa huo zina mashiko licha ya changamoto.

Hata hivyo WHO inasema dalili hizo njema huko Beni na kwingineko zisisababishe watu kubweteka katika harakati za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo kwa kuzingatia kuwa hivi sasa operesheni za kubaini wagonjwa mapema zimekumbwa na mkwamo kutokana na matukio ya ukosefu wa usalama.

WHO kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wake inasema hata hivyo inashirikiana na wadau kuendelea kukabiliana na ugonjwa huo kwa ushirikiano pia na serikali.

Hadi tarehe 8 mwezi huu wa Januari jumla ya visa 628 vya ebola vimeripotiwa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini ambapo 580 vimethibitishwa na kati ya wagonjwa hao, 383 wamefariki dunia.

WHO inasema tahadhari zinachukuliwa kwenye maeneo yote yenye ebola na majimbo mengine nchini DRC na nchi jirani ambapo wanaendelea na ufuatiliaji na uchunguzi.