Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati wa UNFPA wa barubaru na vijana ni muarubaini wa kufanikisha SDGs

Mkakati wa kimataifa wa vijana na barubaru
UNFPA
Mkakati wa kimataifa wa vijana na barubaru

Mkakati wa UNFPA wa barubaru na vijana ni muarubaini wa kufanikisha SDGs

Afya

Shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA limechapisha mkakati wa kimataifa kuhusu barubaru na vijana, mkakati wenye kurasa 31.

Ukipatiwa jina la Mwili Wangu, Maisha Yang una Dunia Yangu, mkakati huo uliotolewa mwezi huu wa Agosti unaweka vipaji, matumaini, mtazamano na mahitaji ya kipekee ya vijana katika kitovu cha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

UNFPA kupitia taarifa kwenye wavuti wake, inasema kuwa “kwa kufanya hivyo, mkakati huo unasaidia kufanikisha SDGs na pia kuweka mipango hiyo iendane na mkakati wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya vijana sambamba na mpango mkakati wa UNFPA wa mwaka 2018-2021.”

Shirika hilo limesema kuwa kila kitu ambacho linafanya kimejikita kwenye ahadi ya kuhakikisha kila mtu anapata haki ya afya ya uzazi na masuala ya kujamiiana kama ilivyobainishwa kwenye mpango wa utekelezaji wa mkutano wa kimataifa wa idadi ya watu na maendeleo, ICPD uliofanyika Cairo, Misri mwaka 1994.

Halikadhalika shirika hilo linasema kuwa kwa kutimiziwa haki zao, vijana wanaweza kuchukua uamuzi sahihi kuhusu miili yao, maish ayao na dunia ambamo kwayo wanaishi na kwamba suala hilo ni haki na kichocheo cha ustawi wao.

Akizungumza kupitia dibaji ya mkakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem amesema mwaka , “leo hii mamilioni ya wanawake na wasichana na baadhi ya wanafamilia wanafurahia maisha bora kutokana na makubaliano ya ICPD. Miaka 25 iliyopita, wanawake wa leo walikuwa wasichana na muongo mmoja baadaye, sisi katika UNFPA tulikuwa na fursa na changamoto za kuambatana na wasichana wengi katika safari yao ya kutoka usichana kuwa watu wazima, wakipita kipindi cha ubarubaru.”

Bi. Kanem amesema kuwa safari hiyo ilikuwa na fursa na vikwazo “hata hivi wasichana walimudu kama ilivyokuwa sisi katika kuwasaidia kufikia uamuzi sahihi wakiwa na taarifa kuhusu haki zao.”

Hata hivyo amesema wao kama shirika la kimataifa wamegundua kuhusu mahitaji pia ya wavulana kupitia sauti na mitazamo yao.

Amesema kwamba “tunafahamu zaidi kuhusu aina ya uwekezaji unaotakuwa kuhakikisha barubaru wanafurahia kipindi hicho na wako tayari kuwa vijana, uwekezaji ambao utakuwa na manufaa si tu kwao bali pia kwa serikali zao katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.”

Ni kwa mantiki hiyo amesema mkakati huo wa UNFPA kwa barubaru utafanikisha malengo ya UNFPA na vijana.