Mkutano wa kamisheni ya idadi ya watu na maendeleo wan’goa nanga UN

1 Aprili 2019

Mkutano wa 52 wa kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo, CPD umeng’oa nanga leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Mkutano huo wa kila mwaka umewaleta pamoja wadau mbalimbali nchi wanachama, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia kujadili mada kuu mwaka huu ambayo niuhusiano baina ya idadi ya watu na juhudi za kufikia malengo ya maendeleo endelevu , SDG’s” lakini pia kusisitiza suala la uwezeshaji wa wanawake.

Kwa kutambua kwamba ukubwa, muundo na mgawanyo wa idadi ya watu duniani una athari katika juhudi za kuchagiza SDG’s kwa juma zima nchi wanachama zinatathimini mwenendo wa sasa wa idadi ya watu, será na mipango ya kamisheni hiyo. Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amina Muhammed amesema, "tangu mwaka 1994 watu wachache ndio wanaoishi katika umasikini uliokithiri, hatari ya vifo wakati wa kujifungua imepungua kwa zaidi ya asilimia 40 na elimu ya msingi imepanua wigo wa matarajio ya mamilioni ya watu lakini bado kuna mapengo katika utekelezaji na bado kuna changamoto nyingi tunazopaswa kuzishughulikia. Juhudi zetu katika baadhi ya malengo ya maendeleo haziendi sanjari na ongezeko la idadi ya watu.”

Mkutano huo pia utaangalia mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa azimio la kihistoria lililopitishwa kwenye mkutano wa kimataifa wa idadi ya watu na maendeleo uliofanyika miaka 25 iliyopita mjini Cairo Misri , mapengo na mapungufu yaliyopo katika kutimiza malengo na matarajio.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa idadi ya watu duniani inakadiriwa kuwa bilioni 7.7 mwaka huu wa 2019 na inatarajiwa kuongezeka na kufikia bilioni 9.7 mwaka 2050, huku umri wa kuishi ukiwa umeongezeka katika mabara yote na kufanya tofauti ya umri wa kuishi baina ya nchi zilizoendelea na zenye maenfdeleo duni ni miaka 15 tu.

Pia Umoja wa Mataifa unasema katika miaka 20 ijayo asilimia 90 ya ukuaji wa miji utakuwa barani Afrika na Asia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter