Hali bado ni tete Msumbiji kufuatia mafuriko:WFP/UNFPA

21 Machi 2019

Hali tete inaendelea katika sehemu kubwa ya Kusini mwa afrika iliyoathirika na kimbunga IDAI kwani mvua kubwa zinaendelkea kunyesha na kusababisha uharibifu mkuwa sababu ya mafuriko umesema leo Umoja wa Mataifa , huku timu za misaada ya kibinadamiu zikifanya kila liwezekanalo kunusuru maisha ya watu na kuwafikia wanaohitaji zaidi msaada.

Likionya kwamba kuna uwezekano mkubwa wa hali kuwa mbaya zaidi shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema watu bado wanahitaji kuokolewa kutoka kwenye paa za nyumba zao baada ya kimbunga hicho kukumba Msumbiji, Malawi na Zimbabwe siku sita zilizopita

Fedha zinazohitajika

Kwa mujibu wa tathimini ya WFP Msumbiji pekee dola zaidi ya milioni 121 zinahitajika ili kusaidia watu milioni 1.7 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. Akiwaeleza waandishi wa Habari mjini Geneva Uswisi hii leo msemaji wa WFP Herve Verhoosel amesema leo Machi 21 serikali ya Maputo imetangaza hali ya dharura “hii ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kutangaza hali hii tangu ilipopata uhuru” Uharibibu mkubwa umefanyika katika miundombinu kama barabara kuu na madaraja ambavyo sasa havipitiki huku nguzo za umeme zimeharibiwa vibaya na kuanguka na hakuna uwezekano wa vikarabati katika wiki kadhaa zijazo.

Kwa mujibu wa taasisi ya taifa ya kuzdhibiti majanga nchini Msumbiji (INGC) zaidi ya watu 100,000 bado wametengwa na hawajafikiwa na msaada wowote katika maeneo ya Chimoio, Dombe na sehemu zingine za jimbo la Manica. WFP inasema kwa kuzingatia kiwango cha dharura yenyewe “WFP inatarajia kuongeza juhudi za msaada hususan katika majimbo yaliyoathirika zaidi huko  Sofala na Manicaambako maelfu ya watu wamepoteza nyumba zao.”

Hali halisi

Shirika hilo limeongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa hali ikazidi kuwa mbaya na idadi ya waathirika ikaongezeka kwani mvua bado inaendelea kunyesha hata sasa. Leo hii WFP imetoa msaada kwa watu zaidi ya 20,000 mjini Sofala, Manica, tete na Zambezi na inalenga kuwafikia watu 600,000 katika wiki nne zijazo. Picha zilizochukuliwa kutoka angani zinaonyesha bonde la Buzi nchini Msumbiji nyumba zote zimesombwa na maji na ndege zisizo na rubani za WFP (drones) zinatumika kusaidia kutambua watu waliokwama, na kutokana na tathimini ya awali ni dhahiri kwamba mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka. “Na kwa sasa sababu tuna taarifa zaidi za hali halisi ni wazi kwamba idadi ya watu laki sita walioathirika itaongezeka katika siku zijazo na hilo litaongeza gharama pia na kama tutawasaidia watu 600,000 kwa miezi mitatu ni gharama ya dola milioni 42, na kama tutahitaji kuwasaidia hadi watu milioni 1.7 kwa miezi mitatu itatugharimu dola milioni 121.5. Bila shaka hatuna fedha hizo.”

Kimbunga Idai kimesababisha uharibifu kwa asimia 90 katika jiji la Beira.
WFP/Andrew Chimedza
Kimbunga Idai kimesababisha uharibifu kwa asimia 90 katika jiji la Beira.

 

Hali ilivyo Zimbabwe na Malawi

WFP inasema nchini Zimbabwe hadi sasa nchini Zimbabwe watu 200,000 wanahitaji msaada wa dharura katika miezi mitatu ijayo.Na kwa mujibu wa WFP wilaya iliyoathirika zaidi ya Chimanimani hali ni taabani kukiwa na asilimia 90 ya nyumba zimeharibiwa vibaya. WFP inasaka zaidi ya dola milioni 5 ili kutoa msaada wa chakula , msaada wa anga na kiufundi kwa ajili ya kufikisha misaada mingine inayohitajika.

Nchini Malawi kimbunga hicho hakikuathiri sana kama nchi zingine . Kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotolewa wiki hii ambapo nyumba 920,000 zimeathirika. Hata hivyo taarifa zinasema watu wameanza kurejea makwao na WFP imeanza mgao wa chakula katika maeneo yaliyoathirika zaidi ya wilaya za Nsanie, Phalombe, Chikwawa na Zomba. Na katika miezi miwili ijayo mpango wa dharura unatarajiwa kufikia watu 650,000 operesheni ambayo inahitaji dola milioni 10.3 kugharamia.

Mchango wa mashirika mengine

Mashirika mbalimbali ya kitaifa, kimataifa na Umoja wa Mataifa yanaendelea kupeleka msaada kadri yawezavyo kusaidia waathirika. Shirika la idadi ya watu duniani UNFPA limekuwa likitoa msaada wa kibinadamu nchini Msumbiji na kuchagiza kulinda afya na mustakabali wa wanawake kwa kupitia huduma za afya ya uzazi na kuzuia ukatili wa kijinsia (GVB).

Baadhi ya msaada huo unaotolewa ni pamoja cliniki za kuhamahama 19 katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika, kutoa makasha 2000 ya kujihifadhi wanawake na wasichana, mahema 3500, kutoka makasha ya huduma ya afya ya uzazi vitakavyokiddhi mahitaji ya watu zaidi ya 300,000 walioathirika na mafuriko ikiwemo vifaa vya kujifungulia kwa jamii na hospitali, vifaa vya matibabu kwa waliobakwa na vile vya kutibu, kukinga na kupambana na magonjwa ya zinaa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter