Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zahma ya mafuriko Msumbiji inaongezeka kwa saa:WFP

Zaidi ya watu 900,000 nchini Malawi na 600,000 Msumbiji wamwathirika kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kutokana na kimbunga IDAI.
WFP/Photolibrary
Zaidi ya watu 900,000 nchini Malawi na 600,000 Msumbiji wamwathirika kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kutokana na kimbunga IDAI.

Zahma ya mafuriko Msumbiji inaongezeka kwa saa:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani linakimbiza msaada wa chakula na vifaa vingine vya muhimu kuwafikia maelfu ya watu waliokwama kutokana na mafuriko makubwa nchini Msumbiji ambayo yanaonekana kuwa zahma kubwa kila saa

Kwa mujibu wa WFP helkopta yake inaendelea kusafirisha biskuti za kuongeza nguvu  , maji, na mablanketi kwa idadi kubwa ya watu ambao wamesaka usalama juu ya paa za nyumba zao na katika maeneo yenyemuinuko nje ya mji wa bandanri wa Beira. Leo pekee tani nne za biskuti zinatarajiwa kuwafikia wahitaji ikiwa ni sehemu ya tani 20 zilizosafirishwa kwenda Beira  kutoka kwenye ghala la akiba la WFP lililoko Dubai.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na kupasuka kwa matawi ya mito miwli sasa yamesambaa katika eneo kubwa na hata nchi jirani ya Malawi na Zimbabwe na kusababisha vifo, uharibifu wa makazi na miundombinu mingine huku maelfu ya watu wakiachwa bila makazi. Herve Verhoosel ni msemaji wa WFP

(SAUTI YA HERVE VERHOOSEL)

"Kimsingi kile wafanyakazi wenzetu wanasema ni kwamba kile wanachokiona ni maji, maji yametapakaa kila mahali, watu ambao wamebahatika wako juu ya paa za nyumba ambako wamebeba mabango ya kuashiria kuomba msaada lakini wengine wengi zaidi ambao hawajabahatika hatuna taarifa kuhusu waliko, kumaanisha kuwa kupata maji na chakula ni ngumu sana na msaada wa jumuiya ya kimataifa ni muhimu sana."

Ameongeza kuwa WFP inaendelea pia kutoa chakula ambacho tayari kimeshapikwa kwenye makazi ya muda ya waathirika wa mafuriko hayo ambao wanahifadhiwa kwenye shule 18 na makanisa mjini Beira na kila kituo kinauwezo wa kuhifadhi watu takriban 1000.

Hofu ya WFP hivi sasa ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwani italeta mafuriko zaidi hasa maji yanayoendelea kujaa kwenye mto mkubwa wa Msumbiji.