Wataalam wa haki za binadamu watoa wito kwa mahakama Misri kusitisha adhabu ya kifo
Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa hii leo mjini Geneva Uswisi wamelaani kitendo cha kuteswa na kuuawa kwa wanaume tisa nchini Misri.
Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu hii leo, watalaam hao wamesema mamlaka za Misri zilitekeleza tukio hilo la kuwaua wanaume hao tisa alfajiri ya tarehe 20 mwezi huu wa Februari na kuwa tayari kulikuwa na rufaa na pingamizi katika mahakama kuu na pia kuwa walilazimishwa kwa njia ya mateso kukiri makosa.
Taarifa hiyo imewanukuu wakisema, "bado tuna wasiwasi zaidi kwamba kesi zingine kadhaa za watu waliohukumiwa zinasubiri mahakamani ,wakikabiliwa na adhabu ya kifo , pia kuna ripoti ya ukosefu wa mchakato sahihi wa kisheria. Hukumu hizi zinaonekana kuwa hazizingatii moja kwa moja sheria na utaratibu wa Misri na kimataifa”
Mwezi Januari mwaka 2018, wataalam walitoa wito kwa Misri kusitisha adhabu za kifo kufuatia ukiukwaji wa haki za binadamu wa mara kwa mara na uonevu.
Ripoti ya haki za binadamu imebaini kwamba tangu kuanza kwa utawala wa Rais el-Sisi mwezi Julai 2013, mahakama ya Misri imekazia hukumu 1,451 za vifo, kati ya rufaa ya kesi 2,443 zilizowasilishwa kutoka mahakama za mwanzo.
Wataalam wameongeza kuwa adhabu ya kifo nchini Misri inaweza kufanyika tu baada ya mchakato wa kisheria ambayo hutoa ulinzi kamili kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, ili kuhakikisha haki inatendeka hadi hukumu ya mwisho.