Dau lilitengenezwa kwa mabaki ya taka za plastiki litasafiri kati ya miji mikongwe ya Afrika Mashariki.

11 Januari 2019

Dau la kijadi lililotengenezwa na taka za plastiki zilizookotwa pwani ya Kenya na miji mbalimbali litaanza safari yake ya kwanza tarehe 24 mwezi huu kutoka mji mkongwe wa Lamu nchini Kenya hadi mji mkongwe huko Zanzibar nchini Tanzania tarehe 7 mwezi ujao, ikiwa ni safari ya umbali wa kilometa 500.

Katika safari hiyo dau hilo litapita na kusimama maeneo mbalimbali ili kuelimisha jamii kuhusu madhara ya taka za plastiki. Na Je nini lengo la dau hili? Kwa nina basi Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili amezungumza na Clara Makenya, mwakilishi wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.

Dau hilo limepatiwa jina la Flipflopi na ni la kwanza la aina yake likiwa na urefu wa mita 9 na limetengenezwa kwa  tani 10 za taka za plastiki. 

Watengenezaji ni kundi linalotaka mabadiliko katika plastiki #PlasticRevolution kwa ajili ya kukabiliana na taka za plastiki ambazo yakadiriwa takribani tani milioni 12 za taka hizo hutupwa kwenye bahari duniani kote kila mwaka hivyo wanahimiza uwezekano wa plastiki hizo kutumika tena.

Akizungumzia dau hilo Kaimu Mkurugenzi wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP  Joyce Msuya  amesema, “Flipflopi ni kielelezo kuwa tunaweza kuishi tofauti. Ni kumbusho kuwa kuna haja ya kufikiria tena jinsi tunatengeneza bidhaa, kutumia na simamia matumizi ya plastiki mara moja. "

Ameongeza kuwa Kenya imeonesha uongozi katika kukabiliana na plastiki zinazotumika mara moja kwa kupinga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. 

Taka hizo ambazo zilitumika kukarabati dau hilo ziliokotwa katika pwani za Lamu ambapo mkarabati mkuu wa dau hilo Ali Skanda amesema, “tunafurahi kuwa tumekarabati boti ya kwanza kutokana na taka za plastiki, kinachofuatia ni kufunga safari na kuwapa watu matumaini katika pwani ya na mbali zaidi kubadilisha mtazamo wa kuona plastiki kama taka bali kama raslimali inayoweza kutumika tena.”

Safari ya Flipflopi kwa ajili ya bahari safi imekuja mwezi mmoja kabla ya kongamano la shirika la mazingira ambapo zaidi ya mawaziri 150 watakusanyika mjini Nairobi, Kenya.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter