Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taka za plastiki zageuzwa vitambaa Burkina Faso

Yassia Savadogo na Ouedraogo Odile wakionyesha baadhi ya nguo nzuri na mikoba inayotengenezwa kwenye karakana yao.
UN Environment/Georgina Smith
Yassia Savadogo na Ouedraogo Odile wakionyesha baadhi ya nguo nzuri na mikoba inayotengenezwa kwenye karakana yao.

Taka za plastiki zageuzwa vitambaa Burkina Faso

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Burkina Faso, wakazi wa eneo la Kougougou lilioko kwenye viunga vya mji mkuu Ouagadougou , wamebuni mbinu mpya ya kubadili taka za plastiki kuwa bidhaa adhimu kama vile mavazi au pochi. 

Wakazi  hao , wanawake kwa wanaume na vijana kupitia kikundi chao kiitwacho NEERE kikimaanisha safi au nzuri, wameamua kugeuza lundo la taka za plastiki zilizosambaa mjini humo kuwa rasilimali muhimu.

Katika karakana yao taka za plastiki ikiwemo mifuko inakatwa vipande vidogo vidogo na kugeuzwa kuwa nyuzi ambazo zinafumwa kuwa kama kitambaa.

Kisha kitambaa hicho hutumika kutengeneza mavazi au mikoba na hivyo kumaliza changamoto ya Burkina Faso ya ukosefu wa udhibiti bora wa taka.

Takribani wanawake 70 wamefundishwa jinsi ya kukusanya, kuchambua, kusafisha na kufuma taka hizo kuwa kitambaa na ni mradi unaoungwa mkono na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP na Muungano wa Ulaya, EU.

Uzi kutoka mfuko wa taka wa plastiki unatumika kufuma kipochi kidogo cha buluu. Kazi hii inafanywa na wanawake na vijana chini Burkina Faso na kusaidia kuwapatia kipato na kusafisha mazingira.
UN Environment/Georgina Smith
Uzi kutoka mfuko wa taka wa plastiki unatumika kufuma kipochi kidogo cha buluu. Kazi hii inafanywa na wanawake na vijana chini Burkina Faso na kusaidia kuwapatia kipato na kusafisha mazingira.

Damien Lankoande, mratibu wa NEERE anasema, “plastiki ni fedha iliyo kwenye mpito kwa sababu iwapo unafahamu jinsi ya kuitumia na kuibadilisha, taka ni fedha. Watu walizoea kutupa plastiki, sasa sisi tunaibadili kuwa mtindo. Kwa hiyo hivi ndio jinsi tumepata jawabu mbadala.”

Mwakilishi wa UNEP kanda ya Afrika Juliette Biao Koudenoukpo, amesema kuwa taka za plastiki ni changamoto kubwa Burkina Faso kwa sababu zinaziba mitaro ya maji, zinaua mifugo.

Kwa hiyo amesema, “wanawake ambao wako kwenye hiki kikundi siyo tu wanatunza mazingira bali pia wanapata kipato na kuleta manufaa kwa jamii zao. Hadi pale suluhisho la kudumu la taka za plastiki litakapopatikana, kwa sasa mifano bunifu kama hii ndio itaendelea kuwa jawabu mujarabu kwa uchafuzi utokanao na plastiki.”

Tangu kuanza kwa kazi hiyo mwaka 2007, kikundi hicho kimesharejeleza tani 2,400 za plastiki na mapato ya mwaka yameongezeka kutoka dola dola 1,120 mwaka 2007 hadi dola 5,620 mwaka huu.