Kuvu anayemeng’enyua plastiki abainika

Kiwango kikubwa cha taka ikiwemo plastiki hutupwa katika mto Nairobi upitao kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi
Picha: Kwa hisani ya James Waikibia
Kiwango kikubwa cha taka ikiwemo plastiki hutupwa katika mto Nairobi upitao kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi

Kuvu anayemeng’enyua plastiki abainika

Tabianchi na mazingira

Hatimaye watafiti wametegua kitendawili cha mioto aina ya uyoga au kuvu inayomeng’enyua plastiki na hivyo kuweka matumaini katika juhudi za kuondokana na plastiki zinazoharibu mazingira.

Watafiti  hao katika bustani za mimea za Kew nchini Uingereza wameripoti kuwa kuvu hao Aspergillus Tubingensis katika wiki chache tu wameweza kumeng’enyua dutu aina ya Polyurethane  inayopatikana kwenye plastiki.

Wakiwa wametoka China na Pakistani, jopo hilo la wanasayansi lilikuwa linasaka jinsi gani linaweza kutenganisha kuvu hao ambao walikuwa wanaweza kumeng’enyua plastiki katika dampo moja kwenye mji mkuu wa  Pakistani, Islamabad.

Wanasayansi katika utafiti wao waliwafuatilia kuvu hao na kuona jinsi ambavyo wanameng’enyua dutu mbalimbali za polymer zilizomo kwenye plastiki katika wiki chache tu badala ya miongo, ikimaanisha kwamba wanaweza kutumika kuozesha plastiki zinakaa muda mrefu kwenye udongo.

Habari hii njema inakuja wakati wakazi wa dunia hii wanahaha juu ya tatizo la utupaji hovyo wa bidhaa za plastiki ambao unaathiri viumbe siyo tu vya nchi kavu bali pia baharini.

Taka za plastiki katika bahari za ni tisho kwa viumbe wa majini
Saeed Rashid
Taka za plastiki katika bahari za ni tisho kwa viumbe wa majini

Mtafiti mwandamizi katika bustani za Kew, Dkt. Illia Leitch anasema “ni vyema kuangalia zaidi kuvu hao. Utafiti zaidi unahitajika kwenye vijiumbe hivi ambavyo vimepuuzwa na penginepo vitatoa jibu la baadhi changamoto kubwa zinazokabili binadamu hivi sasa.”

Amesema kuna zaidi ya aina milioni 3.8 za kuvu lakini ni aina 144,000 pekee ambazo zimetafitiwa na kupatiwa majina.

“Kuna kuvu ndani ya mimea ambao wanaweza kusababisha mimea ikwana mnepo wakati  huu wa mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt. Leitch.

Hata hivyo wataalamu hao katika bustani ya Kew, wanasema “kikwazo kikubwa katika utafiti wa kuvu ni ukosefu wa fedha na ndio maana unakuwa umejikita katika eneo moja au unapungua.”

Kila mwaka takribani tani milioni 8 za plastiki zinaishia baharini na wakati mwingine humeng’enyuka kuwa vipande vidogo sana na hivyo kumezwa tena na samaki na kurejea tena kwenye mnyororo wa chakula, na hadi sasa  madhara ya mwelekeo huu bado hayajafahamika.