Idadi ya waliofikishiwa msaada na WFP nchini DRC mwaka 2018 imeongezeka maradufu

Kadri machafuko yalivyozidi kuenea mwaka 2018, pamoja na idadi kubwa ya watu waliopoteza makazi na kiwango kidogo cha mavuno kilichoambatana na umaskini, hali iliyosababisha idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufikia milioni 13.1, shirika la mpango wa chakula duniani WFP lililazimika kuongeza operesheni zake nchini humo na kufikia watu milioni 5.
Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Kinshasa, DRC, inasema kuwa ongezeko ni maradufu ikilinganishwa na mwaka uliopita wa 2017.
WFP iliongeza msaada wa chakula katika majimbo ya mashariki mwa DR Congo ikiwemo Ituri, Tanganyika, Kivu kaskazini na kusini ambako migogoro iliwalazimisha watu wengi kuyakimbia makazi yao.
Msaada ulitolewa katika mfumo wa bidhaa na fedha, ia vyakula vyenye lishe kwa ajili ya matibabu na kuzuia utapiamlo ambao umewaathiri watoto milioni 4.6 nchini kote.
Kuongezeka kwa misaada ya kifedha kutoka kwa nchi wahisani kumesaidia kuongeza kwa kiasi cha chakula kwa baadhi ya waliokuwa wanalazimika kwa miezi kadhaa kupokea nusu ya kile kilichopangwa.
Mkurugenzi wa WFP nchini DRC, Claude Jibidar amesema, “huu umekuwa mwaka wa majanga mengi na mateso kwa watu wa DR Congo. Tunawashukuru wahisani kwa mchango wao katikakipindi cha uhitaji mkubwa na tunategemea msaada wao kwa mwaka ujao wa 2019 ambao kwa hakika utakuwa na changamoto”
WFP ilipokea misaada kutoka Ubelgiji, Kamisheni ya Muungano wa Uaya, Canada,Finland, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Norway, Korea Kusini, Urusi, Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani.