Wakimbizi wa ndani DR Congo wako katika hali mbaya: UNHCR

14 Disemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, lina wasiwasi na idadi kubwa ya watu ambao wameachwa bila makazi kutokana na mapigano yanayoendelea nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, msemaji wa shirika hilo Charlie Yaxley amenukuliwa leo mjini Geneva Uswisi. 

Amesema machafuko yanayoendelea yanasababisha hata mashirika ya misaada kushindwa kufika katika maeneo kadhaa kutoa misaada ya msingi.

UNHCR inakadiria kuwa nyumba za watu karibu watu milioni 1.5 zimeharibiwa na tathmini hiyo inategemea matokeo ya utafiti wa shirika hilo kutoka katika majimbo 7 saba kati ya 26 ya DRC, utafiti ambao ulifanywa kati ya mwezi mei na novemba mwaka huu wa 2018.

Shirika hilo limesema mapigano makali yakihusisha makundi yenye silaha na vikosi vya serikali na mashambulizi ya kupangwa vimesababisha nyumba nyingi kuteketezwa kwa moto na kuibwa kwa vifaa vya ujenzi na mapaa. “Baadhi ya wale ambao wamelazimishwa kuhama wanaripoti kuwa vijiji vimeteketezwa kwa kiwango cha kuwa majivu,” imesema UNHCR ambapo katika jimbo la Ituri na Kivu kaskazini, inakadiriwa kuwa nyumba 88,000 zimeharibiwa kutokana na vurugu.

Msemaji huyo wa UNHCR ameongeza kuwa, watu wengi wamelazimika kutafuta mahali kwingine pa kuishi ambapo wanalazimika kutegemea familia nyingine kuwapokea na kuwahifadhi. “Hali hii inazidi kuifanya hali iliyokuwa ngumu tayari kuwa mbaya zaidi na kufikia kuwalazimisha wewngine kuingia katika biashara ya ngono au ajira za watoto,” amesema Yaxley.

Ameongeza kuwa katika makazi ya muda watu wako katika hali mbaya wakilala katika vijumba vilivyotengenezwa kwa matawi ya miti na karatasi za plastiki. Wakiwa na ulinzi mdogo dhidi ya watu kutoka nje, wanakabiliwa na magonjwa.

 

Watu waliopoteza makazi yao katika ghasia Ituri DRC.
UNICEF/Madjiangar
Watu waliopoteza makazi yao katika ghasia Ituri DRC.

Mali chache walizobakiwa nazo pia zinaaibwa, wanawake na wasichana wako katika hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili wa kingono. Katika maeneo yaliyoathirika karibu na Beni, Kivu kaskazini, zaidi ya matukio 1,300 ya ukiukwaji wa haki zaa binadamu kwa raia yamerrekodiwa katika miezi mitatu iliyopita, ikiwemo mashambulizi ya mwili, mauaji, uvamizi na utekaji.

UNHCR inasema katika jimbo la Ituri, wiki za hivi karibuni kumekuwa na maashambulizi mapya yaliyofanywa na makundi ambayo hayajafahamika. UNHCR imepokea ripoti kuwa watu wapya 100,000 wamepoteza makazi katika jimbo hilo.

Kwa mujibu wa UNHCR zaidi ya raia milioni moja wa DR Congo hivi sasa wanakadiriwa kuwa wamekuwa wakimbizi wa ndani ya nchi yao kwa mwaka huu wa 2018 pekee.

UNHCR imezitaka pande zote zinazokinzana kuacha mara moja mapigano yanayowalenga raia. Pia shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi limeitaka serikali ya DRC kutatua sababu za watu kuyahama makazi yao na watafute suluhu kwa waathirika.

Msemaji wa UNHCR amehitimisha kwa kuisihi jumuiya ya kimataifa kujitokeza kusaidia hasa kwa kuzingatia kuwa sasa UNHCR imepokea asilimia 46 ya dola milioni 201 zinazohitajika kwa ajili ya shughuli za shirika huko DRC kwa mwaka huu wa 2018 unaoelekea ukingoni.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter