Janga la njaa DRC lafanya nchi hiyo kuwa ya pili duniani kwa njaa baada ya Yemen

2 Julai 2019

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linaongeza kasi ya usaidizi wake kwenye eneo la kaskazini-mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hususan jimboni Ituri kufuatia kuanza tena kwa mapigano ya kikabila yaliyosababisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

WFP inasema janga la sasa la njaa DRC limefanya nchi hiyo kuwa ya pili kwa kuwa na janga la njaa baada ya Yemen kwa sababu watu milioni 13 hawana uhakika wa chakula, milioni 5 kati yao wakiwa ni watoto wenye unyafuzi au utapiamlo uliokithiri.

Vichocheo vya njaa, kwa mujibu wa WFP ni kusambaa kwa mapigano, ukimbizi wa ndani, kupanda kwa bei za vyakula , ukosefu wa fursa za kujipatia kipato, mlo usiokuwa na aina mbalimbali za vyakula, mlipuko wa wadudu wavamizi na magonjwa.

Kwenye jimbo la Ituri, ambako kuna mlipuko wa Ebola, mapigano ya kikabila kati ya wahema na walendu yamechachamaa ambapo katika wiki za hivi karibuni yamesababisha vifo vya watu 160.

Herve Verhoosel ambaye ni msemaji wa WFP mjini Geneva, USwisi amewaambia waandishi wa  habari hii leo kuwa

(Sauti ya Herve Verhoosel)

 “Ukatili huu usio na maana yoyote unafanyika wakati wa msimu wa mavuno, huku wakimbizi wakilazimika kukimbia vijiji vyao na virago kidogo au bila chochote. Manusura wengi wa ghasia hizi ni watu ambao tayari wana utapiamlo na kila mara wanalazimika kukimbia. Hivi sasa wametapakaa na wanasaka usalama maeneo ya mijini au vichakani.”

Licha ya ukosefu wa usalama sambamba na mlipuko wa Ebola kwenye jimbo  hilo la Ituri, WFP inaendelea kusambaza mgao wa chakula kwa walioambukizwa Ebola sambamba na waliokuwa karibuni nao kama njia mojawapo ya kudhibiti mienendo ya wananchi hao.

Mwaka huu pekee, WFP imepanga kuwapatia msaada wa chakula wananchi milioni 5.2 nchini DRC.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud