Skip to main content

Tiba dhidi ya saratani Syria yaimarika kufuatia msaada kutoka Kuwait

Mama kutoka Syria anampa mwanae maji wakiwa Lebanon, mwanae ana saratani, ambapo huduma za afya zinazidiwa uwezo kufuatia idadi kubwa ya wakimbizi.
UNHCR/L. Addario
Mama kutoka Syria anampa mwanae maji wakiwa Lebanon, mwanae ana saratani, ambapo huduma za afya zinazidiwa uwezo kufuatia idadi kubwa ya wakimbizi.

Tiba dhidi ya saratani Syria yaimarika kufuatia msaada kutoka Kuwait

Afya

Nchini Syria msaada kutoka Kuwait umewezesha angalau wagonjwa wa saratani kupata matibabu wanayohitaji na kuwarejeshea matumaini wakati  huu ambapo mapigano yanayoendelea nchini humo yamesambaratisha huduma za afya.

Taarifa ya shirika la afya ulimwenguni, WHO imesema msaada huo wa dola milioni moja kutoka Kuwait umewezesha shirika hilo kununua dawa muhimu za kutibu saratani pamoja na vifaa ambavyo vimesambazwa katika vituo nane vya kutibu ugonjwa huo nchini Syria.

Mwakilishi wa WHO nchini Syria Elizabeth Hoff amesema walishirikiana na hospitali za rufaa nchini humo ili kuandaa orodha ya dawa muhimu zaidi pamoja na vifaa ambapo vilivyopatikana vimepunguza pengo kubwa la matibabu ya saratani yaliyokuwa yanakabili nchi hiyo.

Kabla kuanza mwa mzozo nchini Syria mwaka 2011, huduma za tiba dhidi ya saratani zilikuwa zinapatikana bura katika vituo vyote vya afya.

Hata hivyo mapigano licha ya kusambaratisha huduma, yamesababisha uhaba wa wahudumu wa afya, madaktari na vifaa katika vituo vyote 8 vya kutibu saratani.

“Tayari wahudumu wa afya wa kitengo cha saratani katika hospitali ya watoto mjini Damascus Syria wanasema dawa zimeanza kuleta tofauti kubwa kwa wagonjwa na familia zao,” imesema WHO ikitolea  mfano, mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 11 Yahya kutoka Ghouta ambaye zaidi ya mwaka mmoja uliopita aligunduliwa kuwa na saratani ya damu.

Hata hivyo WHO inasema hivi sasa tiba mahsusi kutokana na msaada wa Kuwait umebadili maisha yake na ana afya njema.

WHO imeshukuru Kuwait kwa msaada huo ambao umeleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya afya hususan kwa kugusa wasyria walio maskini zaidi.