Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za kipato cha juu zina wagonjwa zaidi wa saratani kuliko zile za kipato cha chini.

Mwanamke akipewa tiba ya saratani ya matiti nchini Mexico.
OPS-OMS/Sebastián Oliel
Mwanamke akipewa tiba ya saratani ya matiti nchini Mexico.

Nchi za kipato cha juu zina wagonjwa zaidi wa saratani kuliko zile za kipato cha chini.

Afya

Nchi zenye kipato cha juu zina wagonjwa wengi wa zaidi wa saratani kuliko nchi za uchumi mdogo na wa kati kutokana na mazingira na mitindo ya maisha vinavyoendana na maendeleo ya uchumi na jamii.

Hiyo ni kwa mujibu wa chapisho jipya la taasisi ya kimataifa ya utafiti wa saratani, IARC iliyo chini  ya shirika la fya duniani WHO, ambalo limezinduliwa leo  mjini Lyon Ufaransa likiangazia tatizo la kidunia la ukosefu wa usawa wa kijamii katika suala la ugonjwa wa saratani.

Likipatiwa jina “kupunguza kukosekana kwa usawa wa kijamii katika suala la saratani: ushahidi na vipaumbele vya utafiti” chapisho hilo linaeleza kwa kifupi ushahidi wa kisayansi uliopo, kwa kuzingatia utaalamu wa wakitaalamu wa zaidi ya wanasayansi wa kimataifa wapatao 70 kutoka katika Nyanja mbalimbali.

Mathalani limeonesha ni kwa namna gani tofauti za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kisheria na kiteknolojia zinavyochangia katika kuleta tofauti ya namna watu wanavyoathirika na saratani na ikionesha kuwa watu ambao wako katika hali ya chini wanavyoathirika zaidi.

Tofauti ya athari za saratani katika nchi mbalimbali.

Kiwango cha saratani kwa wastani katika mwaka mzima kwa wanawake na wanaume kwa pamoja ni takribani watu 300 katika watu 100,000 kwenye eneo la Australasia linalojumuisha nchi za Australia, New Zealand, na visiwa vya jirani bila kusahau  Amerika Kaskazini na Ulaya ya magharibi ambapo ni takribani theluthi moja ya hivyo nchini India na katika nchi nyingi katika ghuba ya uajemi nan chi za kusini mwa jangwa la Sahara.

Ingawa kuna idadi ndogo ya aina fulani za saratani katika nchi za kipato cha chini, lakini vifo katika nchi hizo na hata za kipato cha kati vinakaribia kuwa sawa na wakati mwingine zaidi ya vile vinavyotokea katika nchi tajiri, linaeleza chapisho hilo.

Hiyo ni kutokana na uhaba wa kupata huduma za mapema za uchunguzi na matibabu ya mapema. Mzigo mkubwa wa saratani unategemewa kuziangukia zaidi nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Tofauti ya athari za saratani ndani ya nchi.

Imeelezwa kuwa pia kutokana na tofauti za kiuchumi katika jamii ndani ya nchi, athari za saratani zinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.  Chapisho linataja makundi mbalimbali kama vile jamii za asili, makundi ya watu wachache na hata wakimbizi.

Mathalani nchini Colombia wanawake wenye kiwango kidogo cha elimu wako hatarini mara tano zaidi kufariki kutokana na saratani ya kizazi kuliko wanawake wenye elimu ya juu. Nchini Australia,  vifo vya watu wa asili vinavyotokana na saratani kwa pamoja vinakuwa ni asilimia 30 zaidi ikilinganishwa na vile vya watu wasio wa asili.