Saratani ya titi, mapafu na utumbo mpana zaendelea kutesa binadamu- Ripoti

12 Septemba 2018

Zaidi ya wagonjwa wapya milioni 18 wa saratani wameripotiwa mwaka huu wa 2018 huku watu wengine zaidi ya milioni 9.5 wakiripotiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo katika kipindi hicho.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyozinduliwa leo ikipatiwa jina la mzigo wa saratani duniani kwa mwaka huu wa 2018 ikiwa imehusisha takwimu kutoka nchi 185 na kugusa aina 36 ya saratani.

Saratani zilizoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ni ile ya mapafu, titin a utumbo mpana ambapo taasisi ya kimataifa ya utafiti wa saratani, IARC iliyoandaa ripoti hiyo imesema matokeo yanatoafutiana kwa kuangalia chanzo, eneo, aina, sababu za kuenea na hata udhibiti wa ugonjwa huo.

Uchambuzi wa takwimu unaonyesha kuwa idadi ya wanawake wanaopata saratani na kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo ni kubwa kidogo kuliko wanaume huku ikielezwa kuwa idadi ya watu wanaoishi ndani ya miaka mitano tangu kubainika kuwa na saratani inakadiriwa kuwa ni milioni 43.8.

Katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara visa vya saratani ya shingo ya kizazi vimepungua kutokana na huduma za upimaji na ugunduaji wa mapema wa saratani hiyo

Mkurugenzi wa IARC Dkt. Christopher Wild akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva,, Uswisi hii leo wakati wa uzinduzi wa ripoti ametaja sababu za ongezeko la wagonjwa wa saratani kuwa ni uzee, kasi ya ukuaji wa uchumi ambako sasa saratani haiuhusiani na umaskini na maambukizi bali mfumo wa maisha.

Dkt. Wild amesema katika baadhi ya maeneo wamebaini kuwa idadi ya vifo vya wagonjwa wa saratani ni kubwa kuliko kiwango cha ugunduzi wa wagonjwa, akisema hiyo ni ishara ya changamoto katika mifumo au vifaa vya kupima kwa wakati na kuwapatia wagonjwa matibabu.

Wanawake wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha afya cha Kanungu nchini Uganda wakisubiri ushauri na vipimo dhidi ya VVU na Saratani
UNFPA
Wanawake wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha afya cha Kanungu nchini Uganda wakisubiri ushauri na vipimo dhidi ya VVU na Saratani

Hata hivyo wamesema kuna habari njema kwani kwenye maeneo ambako hatua za kinga zimechukuliwa kwa umakini na ufanisi, idadi ya wagonjwa au visa vya saratani imepungua akitolea mfano nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambako visa vya saratani ya shingo ya kizazi vimepungua.

IARC imesema inatiwa hofu pia na ongezeko la saratani ya mapafu miongoni mwa wanawake, “visa vingi vimebainika Amerika ya Kaskazini, Ulaya Kaskazini na Magharibi hususan Denmark na Uholanzi, bila kusahau China, Australia, Newzeland na Hungary.”

“Kanuni njema zilizojumuishwa na mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku zimesaidia kupunguza uvutaji sigara na kuepusha watu kukumbwa na moshi wa sigara maeneo mengi duniani. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa janga la matumizi ya tumbaku linatofautiana katika nchi nan chi ni lazima kuendelea kuweka msisitizo wa sera mahsusi kwa kila nchi,” amesema Dkt. Freddie Bray, Mkuu wa kitengo cha ufuatiliaji saratani, IARC.

Kwa mantiki hiyo Dkt. Wild ambaye ni Mkurugenzi wa IARC amesema takwimu hizo mpya zinadhihirisha kuwa  hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kuepusha mwenendo unaotia mashaka wa mzigo wa saratani duniani akisema  “sera madhubuti za kinga na kubaini mapema ugonjwa huo zinapaswa kutekelezwa ili kwenda sambamba na matibabu na hivyo hatimaye kudhibiti ugonjwa huo unaozidi kuwa janga duniani.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter