WHO yatoa muongozo kukabiliana na maumivu kwa wagonjwa wa saratani
Saratani ni miongioni mwa vyanzo vikubwa vya vifo duniani huku shirika la afya WHO likisema kwa mwaka 2018 ilikatili maisha ya watu milioni 9.6 na kuongeza visa vipya milioni 18.1 kote duniani.
Pamoja na gharama kubwa inayoambatana na gonjwa hilo, kubwa zaidi WHO inasema ni maumivu ambayo huwapata asilimia 55 ya wagonjwa wanaopata matibabu na asilimia 66 ya wangojwa walio katika hatua mbaya za mwisho za maradhi hayo.
Sasa shirika hilo la afya ulimwenguni linasema kwa kiasi kikubwa maumivu hayo ynaweza kupunguzwa kwa dawa na matibabu. Katika kuadhimisha siku ya saratani duniani ambayo kila mwaka huwa Februari 4 ,mwaka huu WHO imeandaa muongozo kwa ajili ya kukabiliana na maumivu hayo makali kwa watu wazima na barubaru.
Lengo la muongozo huo ni kuwasaidia wanaotoa huduma za afya ambao ni pamoja na madaktari, wauguzi, mafamasia na wanaowasaidia wagonjwa kukabiliana na maumivu yatokanayo na saratani.
Kwa mujibu wa WHO muongozo huo pia utawasaidia watunga sera, mameneja wa miradi ya saratani na wahudumu wa afya wa umma kuunda na kuwezesha sera dhidi ya afyunyi na kanuni zinazofanya kazi na salama za kuwaandikia wagonjwa dawa za kudhibiti mauavu ya saratani.
Hii nikutaka kuhakikisha usalama wa wagonjwa lakini pia kudhibiti matumizi mabaya ya afyunyi kwenye jamii.
WHO inasema lengo kubwa la kudhibiti mauavu ya saratani ni kupunguza adha kwa wagonjwa kwa kiwango ambacho kitawaruhusu kuishi maisha yanayokubalika.
Muongozo wa mwisho kutolewa na shirika hilo la afya kuhusu kukabiliana na mauavu ya saratani ilikuwa mwaka 1996.
Muongozo huu wa sasa wa WHO umegawanyika katika maeneo matatu muhimu ambayo ni :mosi kushughulikia chaguo la dawa za kutumia tangu awali kudhibiti maumivu ya saratani, jinsi ya kutoa dawa hizo ikiwemo matumizi ya afyunyi na wakati wa kusitisha, Pili matumizi ya dawa mbadala kama steroids, dawa za kuondoa msongo wa mawazo na nyinginezo na tatu kudhibiti mauavu yanayohusiana na saratani ya mifupa yakijumuisha matumizi ya dawa za kuzuia kulainika kwa mifupa na matumizi ya mionzi.