Mzozo wa Syria ukikaribia kutimu miaka 8, UNICEF yapigia chepuo mahitaji ya watoto

13 Disemba 2018

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta Fore amehitimisha ziara yake ya siku 5 nchini Syria akisema suala la kufikia watoto wote kwenye taifa hilo lililogubikwa na vita kwa takribani miaka 8 sasa linasalia jambo muhimu.

Taarifa iliyotolewa na UNICEF imemnukuu Bi. Fore ambaye ametembelea hospitali na maeneo kadhaa nchini Syria kujionea hali halisi akisema kuwa, “kila mtoto mwenye umri wa miaka 8 nchini Syria amekua katikati ya hatari, uharibifu na kifo.”

Mathalani huko Douma, ambako hatimaye kitendo cha mji kuzingirwa kilikomeshwa na wananchi wakaanza kurejea, Bi. Fore ameshuhudia familia zikiishi na kulea watoto kwenye magofu na katikati ya vifusi huku zikihaha kusaka maji ya kunywa, chakula na jinsi  ya kupata joto wakati huu ambapo ni msimu wa baridi kali.

 “Kuna shule 20, zote zimejaa kupindukia na wanahitaji kufundisha walimu vijana, wanahitaji vitabu, vifaa vya shule, milango, madarasa na umeme,” amesema Bi. Fore.

Akiwa Dera’a, ambako ni makazi ya takribani watu milioni moja, Bi. Fore ameshuhudia adha ya ukimbizi wa ndani ambao unasababisha hata huduma za msingi zisitosheleze wakati huu ambapo nusu ya vituo 100 vya afya jimboni huo vimeharibiwa au vimesambaratishwa kabisa.

UNICEF ikikadiria kuwa watoto milioni 4 nchini Syria waliozaliwa tangu mzozo uanze mwezi Machi mwaka 2011, nusu yao wamekua wakishuhudia na kuona vita. Kwa hiyo Bi Fore anasema, “kuwafikia popote pale walipo na kukidhi mahitaji yao ya sasa na ya baadaye ni kipaumbele chetu kikuu.”

Mkurugezi Mtendaji huyo wa UNICEF ametaja mahitaji hayo kuwa ni elimu, chanjo, ulinzi na wajisikie wako salama.

Akiwa Syria, Bi. Fore amekutana pia na familia na kuzungumza nazo pamoja na jamii ambazo zinawapatia hifadhi wakimbizi wa ndani.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter