Chonde chonde hebu wahamisheni watoto waliokwama Syria kabla hatujachelewa:UNICEF

4 Novemba 2019

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF ametoa wito kwa serikali kote duniani kusaidia kuwahamisha maeffu ya watoto raia wa kigeni waliokwama nchini Syria kabla hawajachelewa na hali kuwa mbaya zaidi.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Bi. Henrietta Fore amesema “ongezeko la machafuko hivi karibuni katika eneo la Kaskazini mwa Syria limedhihirisha haja ya haraka kwa serikali kuchukua hatua ya kuwahamisha Watoto hawa raia wa kigeni kama zahma kubwa haijatokea.Serikali za kitaifa zina wajibu na fursa hivi sasa kufanya maamuzi ya busara, kutenda haki na kuwapeleka Watoto hawa na wazazi wao nyumbaniambako watapata huduma inayostahili na kuwa salama mbali na machafuko na ukatili.”

Kwa mujibu wa makadirio ya UNICEF karibu watoto 28,000 kutoka nchi Zaidi ya 60 ikiwemo Watoto 20,000 kutoka Iraq bado wamekwama Kaskazini Mashariki mwa Syria na wangi wao ni katika makambi ya watu waliotawanywa na machafuko.

“Zaidi ya alisimia 80 ya watoto hawa wako chini ya umri wa miaka 12 na asilimia 50 wako chini ya umri wa miaka 5. Takribani wavulana 250 wengine wakiwa na umri wa miaka 9 tu wanashikiliwa mahabusu ingawa idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi. Wote wanaishi katika mazingira ambayo si mazuri kwa Watoto na swali lao kubwa kwa dunia ni nini kitakachotokea kwetu?. Watoto hawa wanahitaji haraka huduma muhimu na ulinzi.”

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Bi. Fore amesema “tunafahamu kwamba tayari nchi 17 tayari zimeshawahamisha Watoto Zaidi ya 650wengi hivi sasa wanaishi na watu wa familia zao ikiwemo katika maeneo mengine mama zao ambao wamerejea  nao. Watoto wako salama , wanahudhuria shule na kuponya mjeraha ya kiakili yaliyotokana na kushuhudia vita.”

Ameongeza kuwa UNICEF imewasaidia baadhi ya Watoto hawa wanaorejea ikiwemo kuwajumuisha tena na familia zao na katika jamii. Na UNICEF inapongeza uongozi wan chi hizi  na hatua walizochukua na uzoefu wa UNICEF wa kuwasaidia Watoto na familia zao katika maeneo ya vita kote duniani unadhihirisha kwamba palipo na nia pana njia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter