Wasichana wanauwezo wa kuleta mabadiliko, tuwape fursa:UN

11 Oktoba 2018

Wasichana wengi duniani wanakabiliwa na vikwazo katika safari yao ya kuelekea utuuzima, huku mimba na ndoa za utotoni zikiwalazimisha mamilioni kuacha shule na kukatisha ndoto zao. Hivyo umewadia wakati wa dunia kuchukua hatua na kuwapa fursa ya maisha bora wasichana hawa. Wito huo umetolewa na mkurugenzi mtendani wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA, Dkt.Natalia Kanem katika ujumbe kuhusu siku ya kimataifa ya mtoto wa kike.

Dkt. Kanem amesema wasichana hawa hawana sauti hata dhidi ya miili yao, kwani baadhi ya sheria, mila potofu na utamaduni vinawapokonya hadhi na uwezo wao. Na masuala kama ubaguzi wa kijinsia ameongeza , yawawekea msingi  wa kuwakosesha fursa katika maisha yao yote.

Hivyo amesisitiza kuwa mamilioni ya wasichana vigori kote duniani wanasubiri kurejeshewa uwezo wao na kutawala maisha yao na “ni wajibu wetu sote kuwasaidia kufurahia haki zao na kutimiza ndoto zao, hebu tuwekeze katika afya zao na elimu, ujuzi wao na uongozi wao, na kisha tuwaache huru washike hatamu.”

Kwa sababu “tunaamini katika uwezo wa wasichana kuubadili ulimwengu huu kuwa bora zaidi, hebu tuwape nafasi, si lazima wapitie madhila haya, mustakabali tofauti unawezekana na wasichana wenyewe ndio wanaoongoza njia.”

Dkt. Kanem ametaja baadhi ya wasicha hao walio msitari wa mbele kuwa ni pamoja na Tocosana Carlos Jacinto binti wa miaka 14 kutoka Msumbiji ambaye amekuwa mfano wa kuigwa kwa jamii yake kwa kuelimisha wenzie  ambao wengi tayari wameshakuwa mama katika umri mdogo, anawaelimisha kupitia mpango unaoendeshwa na serikali na kufadhiliwa na UNFPA uitwao Rapariga biz. Tocosano anasema” Sauti za wanawake na wasichana zimezimwa, hatuwasikii” na anataka kubadili hali hiyo” nnataka kuwasaidia wasichana kutafuta njia bora na yenye mafanikio”

Nako Malawi amemtaja Jenipher Sanni, aliyetoka kuwa bi harusi mtoto hadi  kiongozi wa vijana na mwanaharakati, hivi sasa anafanya kazi ya kuwasaidia wasichana wenzie kuepuka ndoa za utotoni na kusalia shuleni, wakati yeye mwenyewe akijiandaa kuingia chuo kikuu. Mwaka jana Jenipher alizindua kampeni ya kununu baiskeli 1000 kwa ajili ya kuwasaidia wasicha wa vijijini Malawi kufika shuleni kwa wakati.

Msichana mwingine ni Zahara mwenye umri wa miaka 18 kutoka Uganda ambaye sasa anaelimisha wasichana wenzie kuhusu umuhimu wa elimu akisema kuwa “Baba yangu alifariki dunia 2004…sijui kwa nini nalia, lakini maisha hayakuwa rahisi, ndio maana naelimisha kuhusu elimu kwa washichana, mama yangu hakusoma angalau kama angesoma angeweza kupata ajira, dada ayangu aliamua kuolewa kwa sababu mama hakuweza kutuhudumia tuko sita na mimi ndioye mdogo, na mwengine alipata ujauzito akiwa na miaka 16”

Dkt. Kanem ameikumbusha dunia kwamba zaidi ya yote “kuwasaidia wasichana ni suala la kuheshimu haki zao za kukua, kushamiri na kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wao, lakini pia ni njia ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwetu sote.”

Miongoni mwa wasichana hao ni Zahara mwemye umri wa miaka 18 kutoka Uganda ambaye sasa anaelimisha wasicha wenzie kuhusu umuhimu wa elimu

(SAUTI YA ZAHARA)

“Baba yangu alifariki dunia 2004…sijui kwa nini nalia, lakini maisha hayakuwa rahisi, ndio maana naelimisha kuhusu elimu kwa washichana, mama yangu hakusoma angalau kama angesoma angeweza kupata ajira, dada ayangu aliamua kuolewa kwa sababu mama hakuweza kutuhudumia tuko sita na mimi ndioye mdogo, na mwengine alipata ujauzito akiwa na miaka 16”

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihimiza hilo katika ujumbe wake wa siku hii amesema leo hii vigori milioni 600 wanajiandaa kuingia katika soko la ajira lililobadilishwa na ubunifu na teknolojia, na wasichana hawa wana fikria na suluhu ya nyanja zote za ajira, lakini mara nyingi hawapewi nafasi na fursa wanazohitaji kutimiza malengo na ndoto zao kwa sababu ya vikwazo mbalimbali, ikiwemo ujuzi na mafunzo. Hivyo amesisitiza “Tunahitaji kuwawezesha wasichana kwa elimu inayohamishika na ujuzi wa muda mrefu kama vile fikra, ubunifu na uelewa wa masuala ya kidijitali, na kuwa na watu ambao ni mfano wa kuigwa itakuwa muhimu sana hususan katika ulimwengu wa sayansi na nyanja nyingine ambazo kuna upunguzu mkubwa wa wanawake.

Siku ya kimataifa ya mtoto wa kike huadhimishwa kila mwaka Oktoba 11.

TAGS: Siku ya kimataifa ya mtoto wa kike, UNFPA, Antonio Guterres, SDG’s

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter