Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 40 ya watu duniani wanakabiliwa na uhaba wa maji:Guterres

Maji ni moja ya mahitaji ya msingi ya kuendeleza maisha, lakini kwa wastani watu milioni 117 hawana maji safi na salama katika nchi zinazokumbwa na mgogoro. Picha: UNICEF

Asilimia 40 ya watu duniani wanakabiliwa na uhaba wa maji:Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mtu mmoja kati ya wanne wataishi katika nchi ambako ukosefu wa maji utakuwa ni tatizo sugu na linalojirudia ifikapo mwaka 2050.

Tahadhari hiyo imetolewa  leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres,  akizungumza wakati wa tukio maalumu la kuadhimisha siku maji duniani ambapo pia umezinduliwa muongo wa kimataifa wa maji ili kuchukua hatua kuhusu maji kwa ajili ya maendeleo endelevu SDGs. Guterres ameongeza kuwa

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES )

“Hadi sasa kihistoria maji yamethibitika kuwa ni chachu kwa ajili ya ushirikiano na sio kwa  ajili ya migogoro. Lakini bila udhibiti maalumu wa rasilimali zetu za maji tunahatarisha kuongeza migongano baina ya jamii na sekta na hata kuongeza mivutano miongoni mwa nchi.”

Image
Mwanamke Msomalia anampa mtoto maji katika kituo cha Usajili kwa ajili ya Misaada. Picha: OCHA/Giles Clarke

 

Amesisitiza kuwa maji salama na usafi kwa wote  ambalo ni lengo namba 6 la SDG’s ni muhimu katika kutimiza malengo mengine, na linachangia katika kupunguza umasikini, kukuza uchumi na kuwa na mifumo bora ya maisha.

Guterres amesema ongezeko la uhaba wa maji ni suala la kutia hofu kwani mahitaji yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 40 duniani huku mabadiliko ya tabia nchi yankiongeza shinikizo kwa rasilimali hiyo, na hivyo amesema

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

‘Hatuwezi kuichukulia amani au rasilimali ya thamani ya maji kimzaha. Kwani kwa hakika maji ni suala la uzima na mauati, miili yetu asilimia 60 ni maji. Miji yetu, viwanda vyetu na kilimo chetu vyote vinayategemea rasilimali hiyo.”

Kote duniani hivi sasa zaidi ya watu bilioni mbili hawana fursa ya kupata maji salama na zaidi ya bilioni 4.5 hawana huduma za kutosha za usafi na kujisafi.