Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya IPCC ni kengele ya kutuamsha kuhusu mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati a
Kadir van Lohuizen/NOOR/UNEP
Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati ambapo matumbawe zaidi ya asilimia 99 yanaweza kuwa yametoweka yote katika ongezeko la nyuzi joto 2.

Ripoti ya IPCC ni kengele ya kutuamsha kuhusu mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ameonya kwamba ripoti mpya ya jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ni kengele ya kuiamsha Dunia kuchukua hatua zaidi dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema ripoti hiyo inathibitisha kwamba “mabadiliko ya tabia nchi yanakwenda kasi kuliko sisi na muda unatutupa mkono, tunashuhudia athari kila kona, hali mbaya ya kupindukia ya hewa, kuongezeka kwa kina cha maji, kuyeyuka kwa theluji na kadhalika na wanasayansi wameweka bayana hali halisi ya ongezeko la joto kati ya nyuzi joto 1.5 tofauti na nyuzi joto 2."

Amesisitiza kuwa kiwango cha nyuzi joto nusu kinaweza kuleta mabadiliko makubwa ikimaanisha joto zaidi kwa mamilioni ya watu, kupotea kwa mamilioni ya viumbe, ongezeko la upungufu wa maji, kuendelea kuyeyuka kwa theluji Arctic na kutoweka kabisa kwa matumbawe.

Hata hivyo amesema inawezekana kuepuka zahma hii kwa mujibu wa ripoti, hali itakayohitaji hatua za haraka za kupunguza hewa chafuzi kwa nusu ifikapo 2030 na kufikia uchafuzi sufuri ifikapo 2050.

Lakini amesema hili litahitaji hatua za mabadiliko makubwa katika sekta zote za jamii na hususan zile muhimu kama za ardhi, nishati, viwanda, ujenzi, usafiri na miji.

Na hasa kukomesha ukataji miti na kupanda mabilioni ya miti, kupunguza kwa asilimia kubwa matumizi ya mafuta na kukomesha matumizi ya mkaa kabisa ifikapo 2050. Badala yake kuongeza uwekezaji wa nishati ya upepo, sola, kuwekeza katika kilimo sendelevu na kutoa kipaumbele katika teknolojia safi.

Amehimiza kuwa “Kipindi kijacho ni muhimu sana , ni lazima tutimize ahadi za mkataba wa Paris ili kugeuza kasi hii ifikapo 2020, na mkutano ujao wa Disemba Katowise Poland ni wakati wa kutoshindwa, jumuiya ya kimataifa lazima ije na muongozo muhimu wa utekelezaji wa mkataba wa Paris.”

Ametoa wito kwa nchi zote kufanikisha mkutano wa mabadilko ya tabia nchi wa Katowice akisema “Ni lazima tuishinde changamoto hii ya mabadiliko ya tabia nchi na kufanya wanasayansi wanavyotaka kabla hatujachelewa.”